Thursday, 19 November 2015

ILI nchi yetu isigeuzwe jalala la magari yaliyotumika yasiyofaa kwa matumizi ya barabarani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeanzisha utaratibu wa kukagua na kupima ubora wa magari hayo kabla hayajasafirishwa kuja nchini.
Katika toleo lililopita, safu hii ilizungumzia ukaguzi wa bidhaa zilizo tofauti na magari, lengo likiwa kuhakikisha waagizaji wanafahamu mambo muhimu wanayotakiwa kuyazingatia na kuyatekeleza kuepuka kuingiza kwenye soko la ndani bidhaa zilizo hafifu. Hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoingiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi hawaponzwi na kutokujua kwao au kujitetea kwa sababu ya kutofahamu kwao kuwa bidhaa zenye kiwango fulani cha ubora zinahesabiwa kuwa ni hafifu.
Baada ya kuandika safu iliyopita nikieleza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kukagua bidhaa za nje, wasomaji kadhaa walipenda kufahamu adhabu zinazoweza kutolewa kwa wanaoingiza magari yaliyotumika bila kuyapima ubora na kufanikiwa kuyaendesha katika barabara nchini kinyemela.
Arnold Serukamba, mkazi wa Arusha aliyejitambulisha kuwa ni mfanyabiashara wa nguo maarufu kama nguo za dukani anayefanya biashara katika mikoa ya Kilimanjaro, Pwani na Iringa, Cecilia Irira aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi katika kampuni binafsi inayohusika na masuala ya uchapaji vitabu mkoani Dar es Salaam, pamoja na Anneth Clifford wa mkoani Mwanza, wameuliza maswali kuhusu usafirishaji na ukaguzi wa magari yaliyotumika.
Ingawa maswali yao hayafanani sana, kwa namna fulani yanakaribiana na kunifanya nipate mfululizo mzuri wa kueleza mambo yanayoeleweka kuhusu ukaguzi wa magari yaliyotumika, yanayoagizwa kutoka nje. Wakati Serukamba akitaka kujua endapo tayari TBS imekwishapata wakala nchini Uingereza (UK), Irira alitaka kujua gharama zinazotozwa na mawakala huku Clifford akiuliza kama kuna adhabu yoyote anayoweza kupewa mwagizaji ikiwa ataingiza gari au magari bila kuyakagua ubora.
Clifford aliuliza pia ni kwa nini Serikali ihangaike na hasara za watu wanaoagiza magari kwa kukagua ubora wakati ikiwa ni mabovu wanaoathirika ni waagizaji wenyewe? Nitajibu maswali kama nilivyojibiwa na shirika linalohusika na masuala hayo ya ukaguzi ubora wa magari yaliyotumika (TBS), bila kuzingatia swali gani limeulizwa na nani, ili kutoa elimu kwa mtiririko unaofaa zaidi.
Kwa mujibu wa shirika hilo la viwango nchini, tayari limempata wakala wa kupima ubora wa magari nchini Uingereza (UK) anayeitwa Serengeti Global Services Limited. Kwa maana hiyo, wanaoagiza magari hayo kutoka nchini humo hawana sababu ya msingi ya kutoyapima ubora. Awali ilielezwa kuwa Japan ndio ilikuwa na mawakala pamoja na nchi za Arabuni (United Arab Emirates).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TBS, mawakala waliopo hadi sasa ukiachilia mbali wa UK ni Japan Appraisal Institute Services (JAAI) wa nchini Japan na Quality Inspection Services (QIS) wa nchini humo. Wakala mwingine wa Japan pia ni East Africa Automotive Service Company Limited (EAA). Wakala mwingine ni Jabal Kilimanjaro Autoelect. Mech.
Inspection anayekagua magari hayo yaliyotumika katika nchi za Arabuni. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, mawakala hao wanapatikana kwa zabuni, hivyo wanabadilika kipindi chao cha mikataba kikiisha. Gharama Ili kukagua gari moja lililotumika kwa kutumia mawakala walioko Japan, gharama yake imetajwa kuwa ni dola za Marekani 140.
Kwa ukaguzi wa ubora kwa nchi za Uarabuni gharama ni dola za Marekani 125. Ukaguzi unaofanywa na Serengeti Global Services kwa magari yanayoagizwa kutoka Uingereza ni dola za Marekani 200. Ukaguzi huu hufanywa nchini humo kabla hayajasafirishwa kuja Tanzania. Ofisa Masoko wa TBS, Gladness Kaseka anafafanua kuwa ikiwa gari litaingizwa nchini bila kukaguliwa katika nchi lilikotoka, gharama za kulikagua huwa ni ile inayotozwa kwenye nchi husika pamoja na faini.
“Hiyo ni ikiwa gari limeingizwa kutoka kwenye nchi yenye wakala, bila kukaguliwa ubora. Lakini kwa magari yanayoingizwa kutoka nchi ambazo shirika halina mawakala, ukaguzi wake nchini hufanywa na Shirika la Taifa la Usafirishaji (NIT) bila faini,” Kaseka alisema. Zaidi, Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha TBS, Baptister Bitaho anaeleza kuwa waagizaji wote wanatakiwa kukagua na kupima magari yao katika kampuni hizo kabla ya kuyaleta nchini.
Faini Bitaho anaeleza kuwa, gari lililotumika litakalofika nchini bila kuwa na cheti cha ukaguzi litatozwa faini ya asilimia 30 ya gharama ya ununuzi na usafirishaji (C&F) na pia mwagizaji atalipia gharama za ukaguzi hapa nchini. Inaelezwa kuwa faini huwa ni jumla ya fedha iliyopaswa kulipwa kwa ukaguzi pamoja na asilimia 30 ya gharama ya bima pamoja na ya kusafirisha mzigo au gari husika.
Kiwango cha chini cha faini ni Sh 800,000, hivyo hata kama mwagizaji atakuwa akitakiwa kulipa faini isiyofikia kiasi hicho, atalazimika kulipa fedha hizo kwa sababu ndio kiwango cha chini kilichowekwa kisheria. Shirika hilo limefafanua zaidi kuwa mwagizaji ambaye gari lake litakaguliwa nchini kwa sababu liliingizwa kutoka nchi isiyo na wakala wa kupima, atatakiwa kuilipa NIT Sh 30,000 ikiwa ni ada ya huduma ya ukaguzi, na malipo halalai ya Dola 140 ya ukaguzi wenyewe.
“Wengine wote wanaoagiza magari na kuyaingiza kutoka nchi zenye mawakala wa ukaguzi, bila kuyapima watatozwa gharama halisi ya upimaji na faini,” ilieleza taarifa ya TBS. Sababu za ukaguzi ni usalama na afya ya mwagizaji, mtumiaji na mazingira. Kwa maoni wasiliana na Mwandishi kupitia Simu; 0718836002. email mtegaphilip@gmail.com.

No comments: