PITOMA NEWS ONLINE.BLOGSPOT.COM 14 NOVEMBA 2015
SPIKA wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa kuchaguliwa mjini hapa Jumanne ijayo, ratiba ya Bunge hilo imeeleza. Kutokana na ratiba hiyo, ni wazi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitalazimika kumtaja mgombea wake atakayekuwa na nafasi kubwa ya kuwa Spika kati ya kesho na keshokutwa na kumaliza mvutano wa nani anafaa kuwa spika, baada ya wanachama 22 kujitokeza mpaka jana kuwania nafasi hiyo.
“Kutokana na kuitishwa kwa Bunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli... Ofisi ya Bunge inapenda kuwatangazia wabunge wateule wote kuwa wanatakiwa kuwasili mjini Dodoma Novemba 13, 2015 (jana) tayari kwa ajili ya usajili utakalofanyika bungeni kuanzia siku hiyo hiyo,” imeeleza ratiba hiyo iliyowekwa katika ukurasa wa Facebook wa Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kuanzia jana mpaka kesho, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watapaswa kuwa wameshawasili mjini Dodoma na kujisajili kwa watumishi wa Bunge ambao wameshaanza kazi hiyo.
Baada ya kazi hiyo, ratiba ya Bunge hilo imeonesha kuwa keshokutwa siku ya Jumatatu, wabunge wote wanatarajiwa wawe wameshajisajili ili saa nne asubuhi washiriki kikao cha maelekezo katika Ukumbi wa Bunge kitakachohusisha kutembelea ukumbi huo.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 10 jioni, wabunge hao watakuwa na mikutano ya vyama vyao, ambako inatarajiwa hoja kubwa itakuwa jina la Spika na Naibu Spika.
Spika Siku ya Jumanne wiki ijayo, Watanzania wataelekeza macho yao na masikio katika Kikao cha Kwanza cha Bunge la 11 mkoani hapa, ambacho kitatanguliwa na kusomwa kwa tamko la Rais Magufuli la kuitisha Bunge.
Mara baada ya kusomwa kwa tamko hilo, kutafuatiwa na uchaguzi wa Spika utakaofanyika kwa kura za siri na mshindi akishatangazwa, atakula kiapo siku hiyo hiyo, kisha atapigiwa Wimbo wa Taifa na dua itasomwa.
Siku hiyo hiyo, Spika huyo anatarajiwa kuanza kuapisha wabunge na kazi hiyo ataendelea nayo siku ya Jumatano na kumalizia siku ya Alhamisi asubuhi kwa wabunge watakaokuwa hawajala kiapo cha uaminifu.
Waziri Mkuu, Naibu Spika Alhamisi ya Novemba 16, saa 10 jioni Rais Magufuli anatarajiwa kupeleka kwa Spika jina la Waziri Mkuu ambalo litasomwa mbele ya wabunge wote na kuthibitishwa na wabunge kwa kura.
Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo Naibu Spika atachaguliwa na kula kiapo cha uaminifu na baada ya hapo wabunge watajiweka tayari kwa Hotuba ya Kwanza ya Rais Magufuli itakayotolewa Ijumaa saa kumi jioni na kufuatiwa na kuahirishwa kwa Bunge.
Wabunge wawasili Jana gazeti hili lilishuhudia wabunge mbalimbali wakiingia bungeni na kwenda kusajiliwa katika meza zilizokuwa na watumishi wa bunge hilo. “Umerudi na wewe bungeni? Aaah umemwangusha Waziri ndugu yangu, sikuwezi unatisha sana,” hizo zilikuwa baadhi ya kauli zilizokuwa zikisikika kwa wabunge mbalimbali walipokuwa wakisalimiana mjini hapa.
Kauli hizo zilikuwa zikitumika kwa wabunge wa zamani waliokuwa wakisalimiana wakati wa shughuli ya kujisajili. Wabunge kadhaa walikuwa wakitaniana, huku wakipigana vijembe mbalimbali na wengine wakikumbatiana kwa furaha na kuonesha kushukuru Mungu kwa kuwarudisha tena bungeni.
“Uchaguzi sio mchezo, huko majimboni kuna changamoto nyingi sana, tumetukanwa, tumesemwa vibaya, lakini hatimaye tumeshinda,” alisema Mbunge wa Kavuu, Dk Pudenciana Temba (CCM).
“Sikuwa na sababu ya kuhofia, niliwafanyia wananchi wangu mambo makubwa, barabara sehemu kubwa zinapitika, ndiyo sababu wamenirudisha tena,” alisema Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alipokuwa akizungumza na baadhi ya wabunge wenzake.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), aliwashukuru wapiga kura wake na kusema kuwa kazi yake ndiyo iliyomrudisha tena bungeni. Ngonyani alikuwa akiwapiga vijembe wenzake itabidi afanye utafiti wamerudi namna gani bungeni, huku pia Shabiby akimtania kwamba naye anajua namna alivyowadhibiti wapinzani wake.
Kwa ujumla wabunge wa vyama vyote waliojiandikisha jana walionekana kuwa na furaha na kupongezana kwa namna mbalimbali wakitakiana kila la heri. Kivutio kikubwa ilikuwa kwa wabunge wapya, ambapo watumishi wa Bunge waliokuwa wakipokea wageni walipata wakati mgumu kwa wale ambao hawawafahamu hivyo kulazimika kila wanayemuona kumuuliza kama ni Mheshimiwa au la ili wapate kumuelekeza eneo la kupelekwa.
Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema anashukuru kushinda kwani alipambana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwezeshaji na Uwekezaji), Christopher Chiza na kwamba ilikuwa uchaguzi si wa kitoto.
Bunge la sasa linatarajiwa kuwa na wabunge 393, ambapo ni wabunge wa majimbo 264, huku wa viti maalumu wakiwa 113 na wale wa kuteuliwa na Rais wakiwa 10 wa kutoka Baraza la wawakilishi watano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mmoja.
Bunge la 10 lililomalizika Agosti 21 mwaka huu lilikuwa na wabunge 357, ambapo wa majimbo walikuwa 239, viti maalum 102, wateule wa Rais kumi, Baraza la wawakilishi watano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
No comments:
Post a Comment