PITOMA NEWS ONLINE.BLOGSPOT.COM: 20 NOVEMBA 2015
ALIYEKUWA Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Ackson jana alichaguliwa kwa kishindo kuwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania.
Dk Tulia aliyezaliwa Novemba 23, 1976 wilayani Rungwe, ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais Dk John Magufuli, aligombea wadhifa huo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumshinda Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF).
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema Dk Tulia alipata kura 250 sawa na asilimia 71.2 ya kura zote, huku Sakaya akipata kura 101 sawa na asilimia 28.8 ya kura. Alisema wabunge waliopiga kura walikuwa 351, kati ya wabunge 369 waliosajiliwa kwa ajili ya Bunge hilo.
Wabunge wanaotakiwa kwa mujibu wa Katiba ni 394, lakini idadi hiyo haijakamilika kutokana na sababu mbalimbali.
Baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuapisha Dk Tulia kuwa Naibu Spika, huku akiahidi kumpa ushirikiano na kwamba atafurahia kufanya naye kazi.
Dk Tulia anakuwa Naibu Spika wa kwanza katika siku za karibuni, asiye Mbunge wa Jimbo, lakini akiwa amebobea katika sheria.
Alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na ni mtaalamu katika sheria za hifadhi za jamii, kazi, uhifadhi wanyamapori, udhamini, sheria ya usimamizi wa mirathi, ufadhili miradi na madini.
No comments:
Post a Comment