Friday, 8 April 2016

Hospitali ya Bagamoyo vifaa vya matibabu ni shida tupu.

index
MWENYEKITI wa jumuiya ya wazazi wilayani Bagamoyo,Abdul Sharif,kushoto akimkabidhi vifaa mbalimbali ikiwemo sabuni mgonjwa mzee Sais Selemani ,wakati jumuiya ya wazazi ilipotembelea hospitali ya wilaya ikiwa ni kuadhimisha miaka 61 ya jumuiya ya wazazi kiwilaya.
HOSPITALI ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani,inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa maji hali inayosababisha wauguzi katika wodi ya uzazi kutumia drip katika shughuli zao  pamoja na kuoshea mikono.
Aidha hospitali hiyo inakabiliwa pia na changamoto ya mashuka kuwa machafu kutokana na uhaba wa mashine ya kufulia tatizo linalopelekea mashuka kuganda usaha na damu sanmjali na kutoa harufu mbaya kwenye baadhi ya wodi.
Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya jumuiya ya wazazi ya CCM,wilaya ya Bagamoyo ilipotembelea kujionea matatizo yaliyopo kwenye hospitali hiyo ikiwa ni kuadhimisha miaka 61 ya jumuiya ya wazazi kiwilaya .
Mganga mkuu mfawidhi katika hospitali hiyo,Tumaini Bailon, alisema tatizo la maji linawapa wakati mgumu kwani wanashindwa kufua mashuka kwa wakati huku huduma hiyo ikihitajika zaidi kwa matumizi ya wagonjwa na wauguzi.
Alisema kwasasa maji wanapata mgao mara moja ama mara mbili kwa mwezi huku tanki la maji linalotumika likiwa ni moja ambalo huwekewa maji baridi kwa ajili ya kufulia.
Dk. Bailon alieleza kuwa matanki yalikuwepo mawili lakini kwasasa lipo hilo moja kutokana na jingine kuharibika ambapo walipeleka taarifa katika halmashauri ya Bagamoyo na tatizo linaonekana ni idara ya manunuzi ambayo inakwamisha kutatua tatizo hilo.
Aidha mganga mkuu mfawidhi huyo alisema tanki hilo moja linalotumika ni dogo na ni la lita 5,000 ambalo halitoshelezi kwa matumizi ya hospitali nzima.
“Tatizo kubwa linalotusumbua ni upande wa manunuzi ambao wanakuwa wazito kututatulia maombi yetu hivyo na sisi kushindwa kufanya maamuzi na hatimae wananchi wanapata tabu kama hivi”alisema dk .Bailon.
Alitaja matatizo mengine yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni uhaba wa majengo ikiwa ni sanjali na  vyumba vya waganga wanaohudumia wagonjwa wa kawaida ambapo vipo vinne pekee na  mahitaji ni vyumba saba ili kukidhi mahitaji.
Dk.Bailon alisema katika wodi ya uzazi zipo changamoto nyingi ikiwemo  wodi ilyopo ni ndogo , maji,ukosefu wa umeme ,madawa na net .
Alisema pia wanaupungufu wa watumishi  100 kwani waliopo ni 157 na mahitaji ni zaidi ya 250 ambao wataendana na mahitaji ya hospitali ya kiwilaya.
Alieleza kuwa wanajibana kwa kadri ilivyo ilimradi wagonjwa wapone na kuepusha vifo lakini matatizo ni mengi ambayo yanahitaji ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilayani Bagamoyo,AbdulZahoro Sharif alitoa wiki moja kwa idara ya manunuzi kushughulikia ombi la tanki la maji na endapo wakishjindwa kufanya hivyo jumuiya italinunua.
Alisema watendaji wanapaswa kushughulikia masuala nyeti kwa afya za binadamu badala ya kuyakwamisha jambo linalosababisha malalamiko kutoka kwa jamii.
Sharif alisema wajumbe wa kamati ya utekelezaji na baraza la jumuiya hiyo wamejionea hali halisi na kuchukua changamoto zilizopo hospitalini hapo kisha wanazifikisha katika idara husika ili zifanyiwe kazi.
“Hali ya hospitali ya wilaya ya Bagamoyo inatisha,mashuka yananuka,maji hakuna ,mashuika hakuna na kusababisha wagonjwa kutoka nayo majumbani,madawa watu wananunua nje,umeme hakuna “
“Wodi ya akinamama inakosa umeme kisa nyaya,maji wodi nyeti kama hii haina maji ya kutosha  tena hospitali ya wilaya kuna kila sababu ya kutatuliwa kwa haraka kwa matatizo haya”alielezea Sharif.
Hata hivyo Sharif alieleza kuwa katika kuadhimisha miaka 61 ya jumuiya ya wazazi wametembelea hospitali ya wilaya ya Bagamoyo kujionea matatizo yaliyopo,kutoa baadhi ya vifaa kwa wagonjwa na kupanda miti 1,000 katika shule za sekondari Kingani na Kiaraka.

No comments: