Kufuatia kuendelea kushikiliwa kwa kigogo anayedaiwa kujishughulisha na
biashara ya madawa ya kulevya ‘unga’, Ali Khatib Haji ‘Shkuba’ (pichani)
katika Gereza Kuu la Mkoa wa Lindi, hofu imezidi kutanda kwa madai
kwamba, mfanyabiashara huyo yupo kwenye maandalizi ya kutoroka gerezani
hapo, Uwazi limechimba kwa kina.
BOMBA LA MAJI LATAJWA
Habari zilizolifikia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita na kutiliwa
nguvu na hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea gereza
hilo, zilieleza kwamba, kuna ‘mchongo’ unaofanywa na vigogo kadhaa wa
unga kwa lengo la kumtorosha Shkuba, wakitumia kivuli cha mradi wa
kuingiza bomba la maji gerezani hapo ambapo pengine hata wenye mradi huo
hawajui lolote.
“Kuna bomba linachimbwa kuingia gerezani, wenyewe wanasema ni mradi wa
kulipatia gereza hilo maji lakini kuna tetesi kwamba huenda bomba hilo
ndiyo njia ya kutaka kumtolea Shkuba gerezani lakini wenye mradi hawana
habari.
NJAMA ZAFANANISHWA
“Si unajua hata El Chapo (kigogo maarufu wa unga nchini Mexico),
alitoroshwa kupitia bomba la chooni? Hakuna aliyejua kumbe wenzake ambao
ni Mafia walikuwa wakilipigia hesabu bomba lile la chooni kuja
kushtuka, El Chapo ameshatoka,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la
kutotajwa jina.
Baada ya kupata taarifa hiyo, Uwazi lilianza kufuatilia kwa kina ili
kujua kuhusu mradi huo lakini wakati uchunguzi ukiendelea, Waziri Mkuu
Majaliwa naye alichezwa na machale na kuuzungumzia mradi huo.
Akiwa ziarani mkoani Lindi hivi karibuni, Waziri Majaliwa
alimtahadharisha Mkuu wa Gereza la Lindi, Tusikile Mwaisabila kuwa
makini na zabuni wanazotoa gerezani hapo, ikiwemo ya uwekwaji wa mabomba
ya maji kwani inaweza kutumika kuwatorosha vigogo wa unga, akasisitiza
kwamba ulinzi uimarishwe ili kuhakikisha hakuna kigogo wa unga
atakayetoroka.
MSIKIE WAZIRI MKUU
“…hata hili bomba la maji linalopeleka maji gerezani lisije likawa ni
njia, simamieni sana hili,” alisema waziri Majaliwa akimaanisha
kuimarisha ulinzi katika gereza hilo kwa hofu kwamba watuhumiwa wa unga
wasije wakatumia nafasi hiyo kutoroka.
WAZIRI KITWANGA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga ili kumuuliza kuhusu kudaiwa kwamba mradi huo unaweza
kutumika kutaka kumtorosha Shkuba ambapo alipopatikana kwa njia ya simu
asubuhi na kusomewa maelezo hayo mwanzo hadi mwisho, alimsukumia mzigo
Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, John Minja kwamba ndiye
anayetakiwa kujibu kuhusu mradi huo na hali ya ulinzi gerezani hapo
kufuatia uwepo wa watuhumiwa wa madawa ya kulevya.
“Sasa hilo tafadhali sana muulize Kamishna wa Jeshi la Magereza Tanzania, atakwambia nini kinaendelea,” alisema Waziri Kitwanga.
MSEMAJI WA MEGEREZA
Jitihada za kumpata Kamishna Minja ziligonga mwamba kutokana na simu
yake kutopatikana hewani kila alipopigiwa lakini badala yake,
alipatikana Msemaji wa Jeshi la Magereza Tanzania, Deodatus Kazinja
ambaye kimsingi ndiye mwenye kujua mambo ya magereza yote nchini.
Katika mahojiano na Uwazi, Kazinja alikiri kuwepo kwa mradi huo lakini
akaeleza kwamba wanafuatilia kwa kina kujua ni nani aliyepewa zabuni ya
kuingiza mabomba ya maji gerezani hapo na lini na kuangalia kama kuna
uhusiano wowote kati ya mzabuni huyo na wafanyabiashara wa madawa ya
kulevya walioko gerezani humo.
“Nitafuatilia, nipe muda nijue mradi ulianza lini na nani mwenye zabuni hiyo na uhusiano wake na madai hayo,” alisema Kazinja.
KAMISHNA MINJA KUWASILI
Habari za uhakika kutoka gerezani hapo zinaeleza kwamba siku yoyote
kuanzia Jumapili iliyopita, Kamishna Minja angewasili kwenye gereza
hilo ambapo pamoja na mambo mengine atafuatilia hali ya usalama wa
gereza hilo pamoja na watuhumiwa wa unga waliopo mahabusu.
KIKAO KIZITO CHA GEREZA
Pia, taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema kuwa,
jana Jumatatu, baadhi ya vigogo wa gereza hilo walitarajia kukaa kikao
kizito cha dharura kuangalia mustakabali mzima wa ulinzi gerezani hapo
pamoja na madai kwamba, mradi huo wa kuingiza maji unaweza kutumika
kutaka kumtorosha Shkuba na wenzake.
KAULI ILIYOWAHI KUTOKA
Wiki chache zilizopita, Kamishna Minja alipokutana na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya jijini Dar
alikaririwa akisema:
“Jeshi la Magereza limekuwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kufanya
ukarabati na upanuzi wa magereza za zamani ili yawe na miundombinu
inayoendana na ongezeko la wafungwa na mahabusu.
“Mfano mzuri unapokuwa na mtu kama Shkuba ambaye ni hatari hata kwa nchi
kama Marekani, imetulazimu kuongeza ulinzi katika Gereza la Lindi
ambalo yupo mahabusu mpaka sasa.”
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umedhihirisha kwamba, tangu kauli
hiyo ya waziri mkuu, ulinzi kwenye gereza hilo umeimarishwa maradufu
ambapo askari wengi wameonekana wakirandaranda gerezani hapo kwa saa
ishirini na nne kuhakikisha hakuna ‘figisufigisu’ yoyote inayoweza
kutokea na kusababisha Shkuba na wenzake kutoroshwa.
Shkuba alinaswa saa sita usiku wa Februari 23, 2014 kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar akijiandaa kwenda
nchini Afrika Kusini na kuhusishwa na unga aina ya heroin kiasi cha
kilo 211 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4 uliokamatwa Januari,
mwaka huo mkoani Lindi.
Baada ya kukamatwa, alisafirishwa usiku huohuo kwenda Lindi chini ya
ulinzi mkali wa polisi ambapo Februari 27, mwaka huo aliunganishwa na
watuhumiwa wengine na kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Kusini.
Watuhumiwa hao wengine ni pamoja na binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa
Utumishi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, Maureen Liyumba.
ULINZI KEKO, SEGEREA
Mbali na Gereza la Lindi, ulinzi umeimarishwa pia katika Magereza ya
Keko na Segerea jijini Dar es Salaam ambako vigogo wengine wa unga
wanashikiliwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vyetu makini kutoka katika Gereza
la Keko zinaeleza kuwa, ulinzi ulianza kuimarishwa tangu mwaka jana
baada ya magaidi kutishia kuvamia maeneo yote ya magereza yanayohifadhi
wenzao wakiwemo wale waliohusika kupiga Kituo cha Polisi Stakishari,
Dar.
Mkuu wa Gereza la Keko, Kibwana Sinashida alipohojiwa kuhusu hali ya
usalama gerezani hapo, alisema imeimarishwa na hawana hofu katika hilo.
Kwa upande wa Gereza la Segerea, chanzo kilisema kuwa umeimarishwa kwani hata zana na vitendea kazi vya kisasa vipo vya kutosha.
No comments:
Post a Comment