Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amemueleza Mkuu wa Idara ya
Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sigrifid Kaunala kuwa ni
miongoni mwa watumishi watakaochunguzwa kutokana na kugundulika kuwepo
kwa baadhi ya watumishi hewa waliopata mamilioni ya fedha kama mikopo
kutoka taasisi za fedha.
Mongella alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo ambao pamoja na mambo mengine
alitumia nafasi hiyo kuzungumzia suala la watumishi hewa.
Alisema baada ya uchunguzi wa uhakiki wa awamu ya pili wa watumishi hewa
uliofanywa na Serikali mkoani humo umebaini kuwepo kwa watumishi watano
(majina yao yanahifadhiwa) waliojipatia mikopo ya mamilioni ya fedha
kutoka taasisi za fedha hali inayoonesha baadhi ya mikopo hiyo
isingetolewa bila ya kibali cha waajiri wao.
“Mkuu wa utumishi nasikia hata wewe unahusika kwenye sakata hili la
watumishi hewa, haiwezekani mambo haya yatokee na wewe usijue na wewe ni
miongoni mwa watu tunaowachunguza,” alisema Mongella.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa ya kuhakiki watumishi hewa, Waryoba
Sanya alisema kazi ya kuhakiki watumishi walioko kazini lilianza jana
kwa kuanza na uhakiki wa watumishi wote wa Ofisi Kuu ya Halmashauri ya
Jiji la Mwanza walioko kazini na kuwa lilikuwa linaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment