Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kufanyika kwa
uchunguzi jengo la Machinga Complex kubaini uhalali wa mkataba
uliowezesha ujenzi wa jengo hilo, ikiwa ni pamoja na gharama halisi za
ujenzi.
Alisema hayo kutokana na jengo hilo kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni
36, kiasi ambacho ni mara tatu ya thamani halisi ya jengo hilo na kuleta
shaka ya ufisadi ndani yake. Jengo hilo lina thamani ya Sh bilioni 12.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itaanza kufanya uchambuzi wa
mkataba ili kupata uhalali wa gharama na kujua kiwango kinachostahili
kulipwa na wafanyabiashara hao.
“Katika miradi mingi duniani huu ni wa aina yake, mradi ambao kabla
haujaanza unaweka jiwe la msingi unaanza kudaiwa benki, mpaka unakuja
kumaliza deni lako ni kubwa linakaribia robo mbili au tatu ya mkopo
wenyewe, kabla hata hujaanza kupangisha hata mtu.
“Kwa takwimu zinaonesha tumekopeshwa na jengo limejengwa Sh bilioni
12.7, lakini mpaka dakika hii mnadaiwa Sh bilioni 36 na nyinyi ndio
mnatakiwa kuzilipa, sasa kwa maelezo hayo ndio mnapata picha kwa nini
tumeamua kujipa muda,” alisema Makonda.
Alisema katika maelezo ya awali yanaonesha kuwa jengo hilo lina
mkanganyiko mkubwa na inawezekana kuwa ni miongoni mwa miradi
iliyofanyiwa ufisadi mkubwa.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George
Simbachawene aliifuta bodi inayosimamia jengo hilo na kumsimamisha kazi
meneja anayesimamia jengo hilo na kumtaka kwenda katika ofisi za jiji
kwa ajili ya kumpangia kazi nyingine.
Katika hatua nyingine, Simbachawene alilikabidhi jengo hilo kwa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuwaingiza
wafanyabiashara bila masharti huku ukiangaliwa utaratibu mpya kwa
wafanyabiashara hao.
No comments:
Post a Comment