Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA
Mhandisi Manase Ole Kujan akifungua kikao cha maafisa usafirishaji wa
Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali kilichofanyika leo Jijini
Dar es Salaam Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo
TEMESA Mhandisi Silivester Simfukwe na kulia ni Mhandisi Elirehema
Mmari.
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na
Matengenezo TEMESA Mhandisi Silivester Simfukwe akizungumza na maafisa
usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika
kikao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam kushoto ni Kaimu Mtendaji
Mkuu wa TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan.
Baadhi ya cha maafisa
usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali
wakifatilia kikao kati yao na Wakala wa Umeme na Ufundi(TEMESA)
kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Maafisa usafirishaji kutoka
Wizara, Idara na Taasisi mbali mbali za Serikali wameaswa kuwa wazalendo
kwa kufuata kanuni na utaratibu wa matengenezo na shughuli za kiufundi
Serikalini.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar
es Salaam na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan
alipokuwa akifungua kikao cha maafisa usafirishaji kutoka Wizara, Idara
na Taasisi mbali mbali za Serikali kujadili changamoto zinazowakabili na
kuzipatia ufumbuzi kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zinazosimamia
matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali.
Kaimu Mtendaji Mkuu huyo amesema
kwa hali ilivyo sasa imebainika kuwa Sheria na Kanuni za matengenezo ya
magari na mitambo ya Serikali imekuwa ikikiukwa kwa kiasi kikubwa na
hivyo kuilazimu mamlaka husika kutafuta njia mbadala ili kukabiliana na
changamoto hiyo.
“Lengo letu ni kupata namna bora
ya kutoa huduma ya matengenezo ya kiufundi ya vifaa vya Serikali pasipo
kukiuka Sheria na Kanuni zilizowekwa hivyo basi tunaomba ushirikiano
kutoka kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuleta magari na vifaa
kwetu ili tutekeleze wajibu wetu” alisema Mhandisi Manase.
Mhandisi Manase ameongeza kuwa
pamoja na uchache wa Wizara , Idara na Taasisi za Serikali
zinazotekeleza Sheria na Kanuni za matengenezo ya magari ya Serikali kwa
kuleta magari TEMESA ila kumekuwa na changamoto katika ulipaji wa
gharama za matengenezo hali inayosababisha Wakala usiweze kufanya kazi
kwa ufanisi.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa
Uzalishaji na Matengenezo kutoka TEMESA Mhandisi Sylivester Simfukwe
amesema Wizara , Idara na Taasisi za Serikali zinatakiwa kuzingatia
Sheria na Kanuni zilizopo kwa kupeleka na kulipa gharama za matengenezo
ya magari na vifaa vya Serikali kwani Wakala huu ndio mshauri mkuu wa
Serikali katika masuala ya kiufundi na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo
itasaidia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Naye Meneja Usafirishaji kutoka
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Jonathan Mhagama ameiomba Serikali
kuiongezea uwezo TEMESA kwa kuwa na karakana za kisasa ili kuendana na
mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambapo kwa sasa uwezo walionao
wakala huo ni mdogo ukilinganisha na magari yaliyopo Serikalini.
Mkutano kati ya Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) na maafisa usafirishaji wa Wizara,Idara na Taasisi
mbalimbali za serikali umekuja mara baada ya kauli kutoka kwa Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof Makame Mbarawa ya kuyataka
magari yote ya Serikali kutekeleza Sheria na Kanuni za matengenzo ya
vifaa vya Serikali
No comments:
Post a Comment