SERIKALI ya Wilaya ya Micheweni
Mkoa wa Kaskazini Pemba imekanusha taarifa zilizotolewa na wananchi ya
kwamba vyeti vya kuzaliwa katika Wilaya hiyo hutolewa kwa misingi ya
kisiasa .
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Abeid
Juma Ali aliyaeleza hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara ambao
baadhi yao waliodai kwamba kuna ubaguzi juu ya utoaji wa vyeti vya
kuzaliwa
Alisema kuwa kwa kipindi cha
miezi mitano tangu ashike wadhifa huo tatizo la upatikanaji wa vyeti
vya kuzaliwa kwa watoto katika wilaya hiyo limeanza kupatiwa ufumbuzi .
Alifahamisha kuwa kwa
kushirikiana na watendaji wa Ofisi ya Vizazi na Vifo , ameanza
kulipunguza tatizo hilo , ambapo watoto wengi wameweza kupatiwa vyeti
kwa wakati na bila usumbufu .
“Mtoto hana chama iweje basi
nimbague kwa misingi ya siasa , natambua wajibu na majukumu yangu kwani
mimi ni mtumishi wa umma na ninawatumikia wananchi wote pasi na ubaguzi
”alifahamisha .
Awali mfanyabiashara Ali Salimu
Ali (Baraka) wa Wingwi alisema kwamba kunahitaji kuangaliwa upya Ofisi
inayohusika na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwani imekuwa ikichelewesha
kupatikana kwa vyeti kwa baadhi ya watoto .
Alieleza kwamba wapo watoto
wamefikia umri wa kwenda skuli lakini hawana vyeti vya kuzaliwa , licha
ya kwamba kumbukumbu zao zipo katika Ofisi ya vizazi na vifo lakini
zimeshindwa kufanyiwa kazi .
“Vyeti vya kuzaliwa bado ni
tatizo , kwani kuna baadhi ya watoto wamefikia umri wa kuanza skuli ,
lakini hawana vyeti , tunaomba hii Ofisi inayohusika na utoaji wa vyeti
uiangalie upya nahisi kama kuna ubaguzi fulani hivi ”alisema .
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na
Madiwani wa Wilaya hiyo ambapo Mkuu wa Wilaya alitumia fursa hiyo
kuwataka wafanyabiashara kuwapa ushirikiano wakati wanapokusanya mapato
yatokanayo na biashara zao .
No comments:
Post a Comment