Tuesday, 3 May 2016

NEC YAKAMILISHA RASIMU YA KWANZA YA TAARIFA YA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 2015

lubuva

Kamati Maalum iliyoundwa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kuandaa Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika nchini Oktoba 25, 2015 imekamilisha Rasimu ya kwanza ya Taarifa hiyo na kuiwasilisha kwa Tume.
 
Akizungumza Katika kikao cha Tume mara baada ya kupokea Rasimu hiyo ya kwanza, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mstaafu Damian Lubuva kwa niaba ya Wajumbe wa Tume amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Kamati hiyo licha ya majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Tume hiyo kwa sasa.
 
Jaji Lubuva ameeleza kuwa Tume imeridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa ya kuandaa Rasimu hiyo ikiwa ni pamoja na muda mfupi uliotumika katika kukamilisha kazi hiyo.
 
Aidha, ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa taarifa hiyo inakamilika na kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mapema mwezi Julai mwaka huu.
 
Pongezi hizo pia zimetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bwana Ramadhan Kailima wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa Tume akieleza kufurahishwa kwake na namna ambavyo dhana ya ushirikishwaji ilivyotumika katika kuandaa Rasimu hiyo.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliratibu na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuanzia Otoba 25 mwaka jana na kuhitimisha rasmi zoezi hilo Machi 20 mwaka huu kwa Uchaguzi wa Jimbo la Kijitoupele mkoa wa Kaskazini Unguja.

No comments: