Monday, 14 March 2016

KESI YA WENJE YATIKISA NA KULETA BALAA KATIKA JIJINI LA MWANZA...JIJI LASIMAMA ZAIDI YA SAA MOJA

 
Mamia ya wafuasi wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe leo wamefurika mahakama kuu jijini Mwanza katika kesi ya mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA) anayepinga matokeo ya Stanslaus Mabula (CCM). 

Polisi wametumia nguvu ya ziada kuhakikisha ulinzi unaimarika mahakamani hapo 
 
Ezekia Wenje akiwa Mahakamani 
 
Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula akiwa mahakamani 
 
Ezekiel Wenje akisubiri kutoa ushahidi 

 
 
 
 
 
Freeman Mbowe na Ezekiel Wenje wakiwa mahakamani

Shughuli mbalimbali za kijamii katikati ya jiji la Mwanza zimesimama kwa zaidi ya saa moja,wakati mamia ya wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ) walipokuwa wakitoka mahakama kuu kanda ya Mwanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Nyamagana iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Ezekiel Wenje. 
Wafuasi hao wa CHADEMA walifunga mitaa yote ya jiji la Mwanza, majira ya saa sita mchana wakati wakitoka Mahakamani kusikiliza kesi ya uchaguzi namba 3 ya Mwaka 2016, iliyofunguliwa na Ezekiel Wenje dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo la Nyamagana Mh.Stanslaus Mabula hatua iliyosababisha baadhi ya maduka kufungwa na usafiri wa daladala kusimama kwa muda kwa hofu ya kuibuka vurugu. 


Mwandishi wa Habari hizi ameshuhudia Defender za polisi zikiwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia ( FFU ),wenye silaha za moto na mabomu ya machozi zikifanya doria katika mitaa ya katikati ya jiji pamoja na viunga vya mahakama kuu, ambako tangu asubuhi mamia ya wafuasi wa CHADEMA wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho taifa Mh. Freeman Mbowe walikuwa wamepiga kambi kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo inayosikilizwa na jaji kakusulo sambo. 
Wafuasi hao wa CHADEMA ambao walitoka Mahakamani hapo wakikimbia huku wakiimba na kushangilia kuelekea Hoteli ya Gold Crest,baadhi yao walijikuta wakiwa mikononi mwa Polisi na wengine kupata Mkong’oto na kuswekwa rumande kwa kushindwa kutii amri halali ya polisi iliyowataka kuwa watulivu,jambo ambalo limelalamikiwa na baadhi ya wafuasi hao.
Katika hatua nyingine jaji wa mahakama ya rufaa Mh.Rosemary Ibrahim ametupilia mbali kwa gharama maombi ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa oktoba 25 Mwaka jana, yaliyokatiwa rufaa na wapiga kura wanne wa jimbo la bunda mjini dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Mh. Esther Bulaya,kufuatia makosa ya kisheria yaliyojitokeza kwenye kiapo kilichoapwa na mtu mwingine na kuthibitishwa na mtu mwingine. 
Jaji Ibrahimu amesema Mahakama hiyo imeamua kutoa uamuzi huo kulingana na sheria zinavyoelekeza baada ya wakili wa wapeleka maombi Costantine Mutalemwa na Denis Kahangwa kukiri kuwapo kwa kosa hilo na kutoa mifano ya kesi zilizowahi kuamriwa na mahakama nyingine kwa kuonyesha hazikuwa na makosa kama hayo bali aliyeapa kiapo hicho ndiye aliyethibitisha ila kulikuwa na makosa madogomadogo yaliyokubalika kufanyiwa marekebisho tofauti na hilo.

No comments: