Wednesday, 30 March 2016

UFAFANUZI KUHUSU KIMA CHA CHINI KUHUSU MAFAO YA WASTAAFU PITIA HAPA.

index

TAARIFA KWA UMMA
Hivi karibuni Mamlaka imekuwa ikipokea Malalamiko mengi kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali
wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kuhusu kuwepo kwa tofauti ya kima cha chini cha malipo ya mafao ya wastaafu. Malalamiko haya yanajitokeza kufuatia kutolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 285 la mwaka 2015 kuhusu kupandishwa kwa kima cha chini cha Mafao kwa baadhi ya wastaafu. Kufuatia malalamiko hayo, Mamlaka inatoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
  • Mnamo mwezi Julai mwaka 2015, Wizara ya Fedha kupitia Tangazo la Serikali Na. 285 la tarehe 30/6/2015 (the Public Services Retirement Benefits (Minimum Pensions) Order, 2015 (Government Notice No GN N. 285 of 30/06/2015) baada ya kuridhiwa na Bunge, ilipandisha kima cha chini cha malipo ya mafao kwa wastaafu chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya PSPF. Kwa mujibu wa Tangazo hilo, kima cha chini kwa malipo ya pensheni ya kila mwezi kiliongezeka kwa kiasi cha shilingi 45,000/- pamoja na asilimia 10 ya mafao ya zamani na hivyo kufanya kima cha chini kupanda kufikia kiasi cha takribani Shilingi laki moja (100,000/=).
  • Mamlaka inapenda kufafanua kwamba, ongezeko hilo liliwalenga wastaafu waliokuwa kwenye mfumo wa pensheni wa zamani wa kutochangia (Non-Contributory) wanaolipwa mafao yao na Hazina kupitia Mfuko wa PSPF na HALIKUWAHUSU wastaafu waliopo katika Mifuko ya Msingi (Mandatory Schemes) yaani NSSF, PPF, LAPF, PSPF na GEPF.
  • Aidha, ni muhimu ikaeleweka kwamba, utaratibu wa kuweka kima cha chini cha mafao kwa wanachama wa Mifuko ya Msingi (Mandatory Schemes) yaani NSSF, PPF, LAPF, PSPF, GEPF, NHIF & WCF umeainishwa katika kifungu cha 25 cha Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 kikisomwa pamoja
na kifungu cha 36 cha Sheria hiyo. Kwa mujibu wa vifungu hivyo, kima cha chini cha malipo ya mafao ya wastaafu hupangwa na Mamlaka baada ya kufanya tathimini (Actuarial Valuation) na kushirikisha wadau. Lengo la kufanya tathimini kabla ya kupandisha kima cha chini cha malipo ya mafao ni kujiridhisha juu ya uwezo wa Mfuko husika kubeba ongezeko linalopendekezwa. Kwa kupitia utaratibu huu, mwaka 2014 Mamlaka ilitengeneza na kutoa Kanuni za Uwianishaji wa Mafao (Pensheni Benefit Harmonisation Rules). Kanuni hizi pamoja na mambo mengine zinaainisha kima cha chini cha malipo ya mafao kwa wastaafu kuwa ni asilimia 40 ya kima cha chini cha mshahara wa Sekta husika. Kununi hizi zinatumika kwa Mifuko ya Msingi ambayo ni NSSF, PPF, LAPF, PSPF & GEPF.
  • Vile vile katika jitihada za kuendelea kuimarisha Sekta, Mamlaka imekamilisha zoezi la kufanya tathimini ya Mifuko na Taarifa ya Mtathmini hiyo ipo katika hatua ya majadiliano na wadau wakiwemo wawakilishi wa wanachama. Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo itakuja na mapendekezo mahsusi ya namna bora ya kuboresha mafao ya wanachama. Hivyo, Mamlaka inawasihi wanachama na wadau wengine wote wawe na subira wakati huu ambao taarifa ya Mtathimini inafanyiwa kazi.
Imetolewa na Kitengo Cha Mawasiliano
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846
Tovuti: www.ssra.go.tz
Dar Es Salaam.



No comments: