Serikali inaendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ili kuchangia upatikanaji wa fedha za kusaidia kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imekuwa miongoni mwa taasisi za Serikali ambayo imeanza kukusanya ada zote zitokanazo na huduma inazotoa kwa njia ya kielekroniki kwa wadau wake kufanya malipo kwa njia ya simu au benki kabala ya kupata huduma wanayohitaji.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akiwasilisha mpango wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
“Tayari wilaya 114 kati ya 139 zinakusanya maduhuli kwa njia ya kielekroniki na kwamba ifikapo Juni, 2016 wilaya zote Tanzania Bara zitakuwa zinatumia njia ya kielekroniki kukusanya maduhuli” alisema Dkt. Mwakyembe.
Katika kuongeza mapato, Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa upo mkakati wa kuongeza kiwango cha usajili wa vizazi na vifo nchini, ambapo RITA imeanzisha kampeni ya usajili inayoambatana na uboreshaji wa mfumo wa usajili kwa kuweka mfumo wa kompyuta kila wilaya ambapo kampeni hizo zilifanyika.
Wilaya ambazo kampeni hizo zimefanyika ni Arusha na Arumeru ambapo jumla ya watu 49,548 wamesajiliwa na kupewa vyeti vyao vya kuzaliwa.
Zoezi hilo la usajili linaendelea katika wilaya ya Kahama na baadaye litaendelea katika wilaya 16 nchini ambazo ni Bariadi, Chato, Dodoma, Igunga, Kilombero, Kilosa, Lushoto, Maswa, Mbinga, Misungwi, Mtwara, Muleba, Nzega, Shinyanga, Sumbawanga na Tunduru.
Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa Wizara hiyo kupitia RITA imekusudia kusajili zaidi ya watu 500,000 katika maeneo hayo na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa utafiti wa afya uliofanyika 2010, asilimia 16 ya watoto wenye umri wa miaka mitano ndio wenye usajili na vyeti vya kuzaliwa Tanzania Bara ikilinganishwa na Tanzania Zanzibar ambapo usajili ulikuwa ni asilimia 79.
Ili kukabiliana na hali hiyo, RITA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wamebaini mradi wa kusajili watoto chini ya umri wa miaka mitano uliofanyiwa majaribio wilaya ya Temeke mwaka 2012 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2014 mkoani Mbeya.
Kampeni hiyo imeonesha mafanikio na tija kwa taifa ambapo usajili umeongezeka na kufikia asilimia 58 ambapo awali mkoa wa Mbeya usajili ulikuwa asilimia 8.7.
Kampeni hiyo ni endelevu kwa nchi nzima ambapo mikoa itakayoanza kufanya usajili ni Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Iringa, Njombe, Tabora, Kagera na Dodoma
No comments:
Post a Comment