Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Sista Maria Theleza Ntihabose
wa kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwake
Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita,
kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ameungana na waumini
wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya
Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo pamoja na mambo mengine amewahusia
watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.
“Niwaombe watanzania wote
tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote
tumtangilize Mungu mbele. Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya
kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya
dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya
kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane” Amebainisha Rais
Magufuli
Pamoja na Rais Magufuli na Mkewe
Mama Janeth Magufuli, ibada hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa
Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni
familia rafiki wa Rais Magufuli, waliowasili hapa Chato jana jioni
Tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.
Katika salamu zake kwa waumini wa
Parokia ya Chato, Mheshimiwa Odinga amewashukuru watanzania kwa uhusiano
mzuri walionao na wakenya, huku akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa
mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Mheshimiwa Odinga ametoa mfano
wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya
Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya
nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.
Kuhusu urafiki wake na Rais
Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema urafiki huo ulianza tangu Rais
Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa Waziri mwenye
dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa walibadilishana uzoefu na
kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara, na kwa
umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na waasisi Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Jalamogi Odinga wa Kenya na Milton
Obote wa Uganda. |
No comments:
Post a Comment