Mwenyekiti wa Chama cha Kuhudumia
Watu Wenye Usonji Tanzania (NAPAT) Dkt.Stella Rwezaula(wa tatu kulia)
akiongea na waandishi wahabari kuhusu matembezi ya hiyari kuadhimisha
siku ya usonji Aprilli 16, kushoto ni Katibu wa Chama cha Kuhudumia Watu
Wenye Usonji (NAPAT) Bi. Ella Mgalla na wengine ni wajumbe.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Dk.Abdalla Possi
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika matembezi ya hiyari ya kuazimisha
siku ya watoto wenye usonji Aprili 16 mwaka huu.
Akiongea na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama cha Kuhudumia Watu Wenye
Usonji Tanzania (NAPAT) Dkt.Stella Rwezaula ameeleza kuwa lengo la
matembezi hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu watu wenye matatizo ya
Usonji.
“Jamii imekuwa ikiwanyima uhuru
watu wenye usonji kwa kuwafungia ndani na hivyo kuwanyima haki zao za
msingi ikiwemo kupata elimu ” alisema Dkt.Rwezaula.
Aliongeza kuwa watu wenye
matatizo ya usonji wanapopatiwa msaada wa haraka na unaostahili ikiwemo
huduma ya afya husaidia kuimarisha hali zao na baadaye kuwa msaada
katika jamii yake.
“Usonji ni tatizo linalotokana na
hitilafu katika ukuuaji wa ubongo wa mtoto na kupelekea mtoto kuwa na
matatizo katika mawasiliano na mahusiano ya kijamii na utambuzi lakini
linapogundulika haraka inasaidia kuimarisha hali ya mtoto“ alisema
Dkt.Rwezaula.
Naye Katibu wa Chama cha
Kuhudumia Watu Wenye Usonji (NAPAT) Bi. Ella Mgalla ametoa wito kwa
wazazi kuwasaidia watoto wenye usonji kwa kuwapeleka katika shule
maalum ili waweze kupata elimu.
Pia ameeleza kuwa changamoto
kubwa wanayokumbana nayo ni ukosefu wa waalimu maluum wa kuwafundisha
watoto wenye usonji pamoja na upungufu wa shule maalum ambapo mpaka
sasa kuna shule 8 Tanzania nzima.
“Ninaiomba serikali iweze
kutusaidia kwa kutoa mafunzo maalum kwa waalimu ambao watakuwa
wakiwahudumia watoto wenye matatizo ya usonji na kuongeza idadi ya shule
ambapo kwa sasa ni mikoa minne tu inayotoa huduma hiyo ikiwemo Dar es
Salaam shule mbili, Arusha shule nne, morogoro shule moja na Mwanza
shule moja” alisema Bi.Mgalla
Chama cha Kuhudumia Watu Wenye
Usonji (NAPAT) kimeanzishwa mwaka 2012 kikiwa kinajumuisha wanachama 53
ambao ni wazazi, walezi na waalimu wa watoto wenye usonji.
No comments:
Post a Comment