Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na kulani viakli matukio ya
mauaji ya wazee kumi (10) yaliyotokea wilaya ya Nzega, mkoani Tabora
kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2016.
Inaelezwa kuwa, miongoni mwa
chanzo cha mauaji ya wazee ni imani za kishirikina, uchu wa kumiliki
mashamba na visasi mambo ambayo Serikali imekuwa ikiyakemea vikali.
Wizara inawataka wananchi kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Nzega,
kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa mauaji haya wanakamatwa na kuchukuliwa
hatua kali ili kuwa fundisho kwa watu wengine.
Wizara inasisitiza kwamba wazee
ni binadamu, na wanayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao
kwa mujibu wa Sheria za nchi. Vitendo vya mauaji ya kikatili
wanavyofanyiwa wazee vinasababisha hofu kubwa kwa wananchi. Mauaji hayo
yanawakosesha amani na vinadhohofisha ari ya kufanya shughuli za za
maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla. Familia inayoishi na mzee
anayewindwa, itatumia muda mwingi kutekeleza jukumu la ulinzi na hivyo
kupunuza tija na uzalishaji wa mwananchi mmoja na familia kawa ujumla.
Kwa kutambua hili Wizara inahimiza wadau wote kuunga mkono jitihada za
Serikali katika ulinzi wa wazee na kuboresha huduma zao ili kuelekeza
nguvukazi katika uzalishaji.
Wizara inapenda kutoa pole kwa
familia ambazo zimeguswa na mauaji ya wazee waliopoteza maisha kwa
kuuawa kinyama. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wazee wana haki ya
kuthaminiwa utu wao, kupata huduma stahiki, na kushiriki haki zote za
msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo
haki yao ya kuishi. Aidha, Jamii ihakikishe kuwa wazee na wananchi wote,
wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu kwa ajili ya
maendeleo na ustawi wa Taifa letu.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
15/4/2016.
No comments:
Post a Comment