Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Felix Lyaniva
ametoa wito kwa wanarorya wanaoishi Jijini Dar es salaam kuwekeza kwenye
fursa zilizopo katika wilaya hiyo iliyopo mkoani Mara.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa wanarorya
wanaoishi Da es salaam utakaofanyika katika ukumbi wa Karimjee siku ya
jumapili Februari 17, 2016 kuanzia saa nane mchana.
“Wilaya yetu ya Rorya ina fursa nyingi za
uwekezaji zikiwemo za biashara, ardhi yenye rutuba, gesi asilia, mifugo
pamoja na misitu, lakini pamoja na kuwa na fursa za rasilimali zote hizo
bado ni miongoni mwa wilaya ambazo ziko nyuma kimaendeleo hivyo
tunahitaji wanarorya wachukue hatua” alisema Mhe. Lyaniva.
Mhe. Lyaniva ameongeza kuwa licha ya wilaya
ya Rorya kupiga hatua na kuwa Halmashauri haijawa na kasi ya
kuridhisha kutokana na wanarorya waishio nje ya wilaya hiyo kutoshiriki
ipasavyo kwenye fursa za kiuchumi na kwenye utatuzi wa changamoto
mbalimbali zinazoikabili wilaya hiyo.
Aidha, Mhe. Lyaniva ameelezea baadhi ya
changamoto zinazowakumba wananchi wa Rorya zikiwemo za ugonjwa wa
Ukimwi, njaa pamoja na ukosefu wa huduma bora za kijamii kama vile maji
safi na salama, barabara, Hospitali, shule, vyuo vya ufundi pamoja na
vituo vya kutosha vya ulinzi na usalama kwa upande wa Jeshi la Polisi.
Kabla ya mwaka 2007 Rorya ilikua sehemu ya
Wilaya ya Tarime, kwa sasa Rorya imekua wilaya mojawapo kati ya wilaya
nne zilizopo Mkoani Mara
No comments:
Post a Comment