Friday, 15 April 2016

Watumishi HEWA Jijini Arusha Waongezeka na Kufikia 300.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema idadi ya watumishi hewa mkoani humo imeongezeka baada ya uchunguzi wa awali huku baadhi ya waliokuwa wakifuja fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba kuzirejesha.

Aidha, amesema mkoa umepoteza Sh bilioni 1.8 kwa mwaka jana kutokana na kulipa watumishi hewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini  Arusha, Ntibenda alisema hivi sasa mkoa huo unafuatilia akaunti za watumishi hao hewa ili fedha hizo zirudishwe serikalini huku watumishi wengine baadhi waliokuwa wakifuja fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba kuzirejesha.

Alisema awali wakati timu ya uchunguzi aliyoiunda kuchunguza watumishi hewa ilibaini mkoa huo kuwa na watumishi hewa 270, lakini hadi jana idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya 300.

Alisema wilaya mbili za Karatu na Arumeru ndizo ambazo watumishi hewa wameongezeka.

“Bado tunaendelea na uchunguzi na naamini wataongezeka lakini hivi sasa hao watumishi hewa wanahaha kurudisha fedha za serikali lakini hata kama wakirudisha watapelekwa mahakamani,” alisema Ntibenda.

Alisema hata kama fedha hizo watazirudisha, lakini watawafikisha mahakamani na pia wanafuatilia kujua ni kwa nini wakuu wa idara zao walifahamu udhaifu huo, lakini walikaa kimya na kuwalipa mishahara huku wakijua kuwa wanaihujumu serikali.

Alisisitiza ni vyema watu wakaacha tabia ya kujipatia fedha nyingi kwa njia isiyo halali kwani watumishi hewa wanasababisha fedha za serikali kushindwa kufanya shughuli nyingine badala yake kupata hasara.

Katikati ya mwezi uliopita, wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wapya, Rais John Magufuli aliagiza waende kufuatilia watumishi hewa katika mikoa yao na hadi sasa wamegundulika watumishi hewa zaidi ya 4,000.

No comments: