Wanachama
wa Chama cha Wananchi (CUF), wameanza kushikana uchawi, huku viongozi
wakitakiwa kutoa maelezo ya kwanini wameshindwa kujadili hatua ya
kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba.
Pamoja
na hali hiyo, wanachama hao wamemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho,
Maalim Seif Sharif Hamad kutambua kuwa ana wajibu wa kuwasiliana na
Profesa Lipumba ili arejee katika nafasi yake ya zamani kwa mujibu wa
katiba ya chama hicho.
Hayo
yamesemwa Dar es Salaam jana, wakati wa kongamano lililoandaliwa na
Kata ya Makurumla Manispaa ya Kinondoni, ambapo mmoja wa wana CUF
Mohamed Mgomvi, alisema anashangazwa na hatua ya kikao cha Baraza Kuu
kushindwa kujadili barua ya kujiuzulu Profesa Lipumba.
Alisema CUF kwa upande wa Bara, imebaki haina mtu madhubuti ambaye anaweza kukiendesha kama alivyokuwa kiongozi huyo.
“Ninashangaa
hapa mzee Wandwi (Mustafa), kama Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
chama unashindwa kusema ukweli. Leo hii (jana) CUF imebaki yatima tangu
alipoondoka Profesa Lipumba halafu mnasema tupo naye pamoja.
“Haiingii
akilini hata kidogo, ni unafiki umetawala kwa baadhi ya viongozi ambao
kila kukicha wanakutana na Lipumba wanamuonyesha wanamhitaji, akitoka
mnamsema vibaya.
“…napenda
kukuambia leo CUF hakuna mwenye uwezo wa kuvaa viatu vya Profesa
Lipumba tunamhitaji kiongozi wetu, tumechoka kuburuzwa na unafiki
unaoendelea ndani ya chama,” alisema Mgomvi.
Naye
Mangaa Dachi, alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF barua ya kujiuzulu
Profesa Lipumba inatakiwa iwasilishwe katika kikao cha mkutano mkuu
uliomchagua kuliko ilivyo sasa.
“Hivi
mnajua kama chama tunavunja Katiba? Kama ndivyo hivyo bado suala la
Profesa Lipumba linatakiwa kuwasilishwa kwenye mkutano mkuu, nasi
tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake,” alisema Dachi.
Pamoja
na hali hiyo wanachama hao walilalamikia mfumo wa upatikaji wa wabunge
wa viti maalumu ndani ya chama hicho kuwa umekuwa ukihusishwa na tuhuma
za rushwa kwa baadhi ya wakurugenzi.
“Hatuwezi
kuvumilia hali hii hata mfumo wa upatikaji wa wabunge wa viti maalumu
hivi sasa watu wanafanya wanavyojisikia, leo kuondoka kwa Lipumba wapo
baadhi ya wakurugenzi wanatajwa kuchukua fedha kutoka kwa baadhi ya
wabunge waliopo sasa ili wawape ubunge,” alisema.
Akifungua
kongamano hilo, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Mustafa Wandwi,
alisema pamoja na yanayoendelea bado wako pamoja na Profesa Lipumba kwa
kila jambo linaloendelea ndani ya chama hicho.
Alisema
kutokana na hoja ya washiriki wa kongamano hilo, bado kuna kila sababu
ya kutafakari kwa kina suala la Profesa Lipumba lakini hata katika kikao
cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika hivi karibuni visiwani
Zanzibar, suala hilo lilijadili kwa kina.
No comments:
Post a Comment