Monday, 18 April 2016

TIMU YA UCHUKUZI HAINA MAMLUKI Jua inaendeshwa na nani jibu lipo Hapa.

1 
Wachezaji wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC wakifanya mazoezi ya viungo kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.

2 
Wachezaji wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC wakisikiliza maelekezo ya kocha Judith Ilunda (mwenye tisheti nyeupe anayetazama kamera).
3 
Mchezaji Subira Jumanne wa Uchukuzi SC akiwahi mpira.

TIMU ya Uchukuzi SC imesema haina wachezaji mamluki watakaowatumia katika mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza Jumatatu (Aprili 18), kwenye viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Uchukuzi SC, Mohamed Ally, alisema jijini hapa kuwa hawawezi kutumia mamluki kwani ni moja ya masharti na kanuni ya mashindano hayo, kwani hairuhusiwi kutumia wachezaji ambao sio waajiriwa wa taasisi au wizara zinazoshiriki kwenye mashindano hayo.
“Tumekuwa tukishiri haya mashindano na mengine mengi yanayoshirikisha taasisi za serikali na moja ya masharti makubwa ni kutotumia wachezaji wasiokuwa wafanyakazi halisi wanatambulika kama mamluki, hili tulisimamia kwa kuhakikisha wafanyakazi waajiriwa katika idara mbalimbali ndio wanaocheza katika mashindano haya” alisema Ally.
Ally alisema wanawachezaji wengi wenye viwango vya juu, ambao wanauhakika wa kufanya vizuri kwa kuchukua ubingwa katika michezo mbalimbali baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
“Tuliweka kambi kwa takribani miezi miwili huku tukifanya mazoezi kwenye viwanja vyetu vilivyopo kando kando ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na baadaye tukacheza mechi za kirafiki na timu mbalimbali za soka ikiwemo Amadori Boys ya Pugu Sekondari,” alisema Ally.
Naye kocha wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC, Judith Ilunda alisema hana hofu na wachezaji wake kutokana kufanya mazoezi ya kutosha kwa kucheza mechi tatu za kitafiki na timu za Uhamiaji na Cargo.
“Tunauhakika wa kutwaa kombe kwa sababu tumefanya maandalizi kabambe na tuna wachezaji wazoefu, wakiwemo waliowahi kuchezea timu ya taifa na wengine bado wapo katika timu hiyo ya taifa,” alisema Ilunda mchezaji wa zamani wa timu machachari ya Bandari na timu ya taifa.
Aliwataja baadhi ya wachezaji hao wazoefu ni pamoja na Matalena Mhagama, Mwadawa Hamisi, Subira Jumanne, Mary Kajigili na Sharifa Mustafa.
Meneja na kocha wa timu ya soka ya Uchukuzi SC, Robert Damiani alisema wapo tayari kwa mashindano kutokana na maandalizi kamambe waliyoyafanya wakiwa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa timu ya riadha wa Uchukuzi SC, Kingsley Marwilo alisema atakuwa wachezaji watatu wa marathoni, ambao ni Scolastica Hasiri, Ramadhani Mwakilongo na Leonard Julius.
Timu ya Uchukuzi SC, ambayo inashiriki kwenye michezo ya soka, netiboli, riadha, baiskeli, kuvuta kamba, karata, bao na vishale, mwaka jana ilitwaa vikombe 13 kati ya hivyo vitano vilikuwa vya ubingwa wa kwanza, na vilivyosalia vilikuwa vya ushindi wa pili na tatu

No comments: