Mkuu wa Wilaya ya Butiama,
Annarose Nyamubi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, juzi
alimzuia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba kwenda kijiji
cha Mikomario wilayani Bunda kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi
na mwekezaji kwa madai ya wasiwasi wa usalama kuwa mdogo.
Baada ya
jitihada zake za kumzuia kugonga mwamba, Nyamubi ambaye pia ni Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Bunda aliamua kujitenga na ziara hiyo kwani licha ya
kufika eneo la mkutano, hakujihusisha na lolote kwa kuamua kukaa
pembeni.
“Mheshimiwa waziri nakushauri usiende Kijiji cha Mikomario kwa
muda huu ambao unakaribia usiku kwa sababu usalama utakuwa ni mdogo
kutokana na ukorofi wa wananchi wa eneo lile,” alishauri Nyamubi wakati
akizungumza na Nchemba ofisini kwake.
Hata hivyo, waziri Nchemba
alisisitiza kuwa lazima aende kuzungumza na wananchi hata kama
atalazimika kuhutubia kwa kutumia taa za gari kwa sababu aliwaahidi kuwa
angefika na kuzungumza nao na walikuwa wakimsubiri tangu mchana.
“Mheshimiwa kaimu mkuu wa mkoa, bado sijashawishika kutotimiza ahadi ya
kwenda kuzungumza na wananchi wale, wamenisubiri tangu asubuhi na
nimepata taarifa wako uwanjani hadi jioni hii wakinusubiri. Kutokwenda
ni kutowatendea haki,” alisisitiza Nchemba.
Baada ya msimamo huo, ndipo
Nyamubi alipotangaza kujitoa kwa lolote ambalo lingetokea, licha ya
kuwamo kwenye msafara wa viongozi uliofika kijijini hapo saa 12.40
jioni, hakukaa meza kuu wala kujishughulisha na lolote hadi mkutano
ulipomalizika kwa amani saa 1.10 usiku.
Akizungumza na wakazi wa kijiji
hicho ambacho kimekuwa na mgogoro wa ardhi kwa miaka 30 sasa bila
ufumbuzi, Waziri Nchemba aliahidi kuutafutia ufumbuzi, lakini akawasihi
kuwa na subira kwa sababu lazima awasiliane na wizara nyingine
zinazoguswa nao.
“Suala hili ni la kisheria, hivyo linatakiwa
kutatuliwa kisheria badala ya mapigano, nipeni fursa ili wizara yangu
iwasiliane na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na
Tamisemi ili kwa pamoja tuutafutia ufumbuzi.
“Wenye mamlaka ya kupanga
na hata kubadili matumizi ya ardhi ya kijiji ni ninyi wananchi kupitia
mikutano na Serikali yenu ya kijiji, viongozi na wataalamu kazi yetu ni
kutoa ushauri kuhakikisha uamuzi wenu unakuwa halali,” alisema.
Wakiwa
na mabango yenye ujumbe, wakazi hao walimpongeza waziri kwa kutimiza
ahadi ya kuzungumza nao ili kutafutia ufumbuzi mgogoro huo unaohusu
hekta 2, 500 zinazodaiwa kutolewa kwa mwekezaji bila ridhaa ya Serikali
ya Kijiji.
No comments:
Post a Comment