Thursday, 12 May 2016

Kibarua cha Rais wa Brazil Chaota Nyasi, Apigiwa Kura ya Kutokuwa na Imani Naye.

Kitumbua cha Rais wa Brazil, Bi. Dilma Rousseff kimeingia mchanga.

Baraza la senate limempigia kura ya kutokuwa na imani naye. Hiyo inamaanisha kuwa atakaa benchi na kupelekwa kortini. Bi Rousseff anatuhumiwa kulaghai hesabu za kifedha ili kuficha deni la umma linalokua kabla ya uchaguzi wa mwaka 2014, kitu anachokanusha.

Maseneta walipiga kura 55 za kumuondoa katika mkutano uliodumu kwa zaidi ya saa 20. Ni 22 tu ndiyo waliokuwa upande wake. Makamu wa Rais, Michel Temer atakaimu nafasi yake wakati kesi ya Bi Rousseff ikianza kusikilizwa.

Kesi hiyo inaweza kuchukua siku 180 hiyo inaamanisha kuwa atakuwa amesimamishwa katika kipindi ambacho michuano ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro itaanza, August 5.

No comments: