Dodoma. Mahakama ya Rufani itasikiliza rufaa 40 na kutoa hukumu katika vikao vyake vinavyoendelea mjini Dodoma.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Eddie Fussi alisema jana kuwa vikao hivyo vilianza Aprili 4 na vitamalizika 29.
“Rufani zitakazosikilizwa ni kesi za mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, ubakaji na wizi wa mifugo,” alisema Fussi.
Alilitaja jopo la majaji watakaosikiliza rufaa hizo kuwa ni Engela Kileo (Mwenyekiti), Catherine Orio na Profesa Ibrahim Juma.
Miongoni mwa rufaa ambazo tayari zimesikilizwa ni ya Said Sui, ambaye
alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Singida kutumikia kifungo cha miaka
30 jela baada ya kutiwa hatiani mwaka 2012 kwa kosa la kubaka.
Jaji Kileo alihoji uhalali wa jalada la kesi hiyo kutoeleza sababu za mahakimu watatu kubadilishana.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Morice Sarara aliiomba Mahakama
hiyo kufuta hukumu iliyotolewa na kuirejesha kesi hiyo Mahakama ya
Wilaya ya Singida ili hakimu aliyeanza kuisikiliza aendelee pale
alipoishia. Mkata rufaa, Sui alikubaliana na maelezo ya Wakili Sarara na
kwamba hana pingamizi kwa kesi hiyo kurejeshwa Mahakama ya Wilaya ya
Singida kuendelea kusikilizwa alipoishia hakimu wa mwanzo. |
No comments:
Post a Comment