Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Kigoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye amekiri kwamba Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, aliyoitumia
kulifuta Gazeti la Mawio ni mbaya inahitaji kufanyiwa marekebisho.
Akizungumza na wadau wa sekta ya wizara yake mjini Kigoma ,Nape amesema
sheria hiyo iliyokuwa ikilalamikiwa na wadau wa habari kwa miaka mingi,
sasa muswada wake utapelekwa bungeni ili ujadiliwe na kufanyiwa
marekebisho.
Muswada huo utakaojulikana kama Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari,
utakuwa chini ya wizara hiyo huku Muswada wa Haki ya Kupata Habari,
utawasilishwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Ili kuondoa manung’uniko kwa waandishi na habari, wizara hiyo itaunda
Bodi ya Kusimamia Maadili, Miiko na Uendeshaji wa Vyombo na kusimamia
mwenendo mzima wa waandishi kama ilivyo kwa bodi za makandarasi au
madaktari.
“Kama ni adhabu zitatolewa na nyie wenyewe kupitia bodi yenu, bila shaka itasaidia kupunguza makanjanja,” amesema Waziri Nape.
Amesema muswada huo umezingatia maoni ya wadau kwa asilimia 99 ya
mapendekezo yao, hivyo ni unaakisi kile kilichokusudiwa na waandishi wa
habari na wadau wa sekta hiyo nchini.
Pia, amezitaka halmashauri za wilaya na manispaa kuanzisha vituo vya
utangazaji, ili watoe taarifa nyingi za maendeleo kwa watu na
kuhamasisha ukusanyaji mapato ya halmashauri.
Waziri Nape ameagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuajiri maofisa habari
kila halmashauri, wahakikishe wanashiriki vikao vyote vya uamuzi hata
kama siyo wajumbe lakini waingie kama waalikwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga
amesema mkoa una maofisa habari wanne ilhali mahitaji ni tisa, jambo
linalokwamisha utoaji taarifa kwa wananchi.
Jenerali Maganga ameomba wizara kuagiza vituo vya redio na runinga
kuandaa vipindi vya kuelimisha jamii, badala ya burudani hivyo kujikuta
wananchi wakikosa fursa nzuri ya kujifunza njia bora za kujikwamua na
umaskini.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Kati, Eswatie
Masinga amesema mamlaka imejipanga kutoa adhabu kwa vituo vya utangazaji
vinavyotumia maudhui yasiyozingatia maadili, hivyo kwenda kinyume na
utamaduni wa Mtanzania.
Masinga amesema Kigoma umepangiwa nafasi nane za kuanzisha vituo vya
utangazaji, kila wilaya imepangiwa nafasi mbili, akitaja wilaya
zitakazonufaika na mpango huo kuwa ni Kigoma, Kasulu, Uvinza na Buhigwe. |
No comments:
Post a Comment