Haji Manara-Afisa habari Simba SC
Mkuu wa kitengo cha habari wa klabu ya Simba SC, Hajji Manara
ameiomba Taasisi ya Kupambana na Kuzia Rushwa nchini-TAKUKURU kuweka
kambi na kufanya uchunguzi yakinifu katika Shirikisho la soka nchini,
TFF ambalo limegubikwa na tuhuma za rushwa na upangaji matokeo katika
michezo miwili ya mwisho katika ligi daraja la kwanza.
Jumapili iliyopita Kamati ya nidhamu ya TFF ilitoa hukumu ya tuhuma za
upangaji matokeo zilizokuwa zikizikabili timu za Polisi Tabora, JKT
Oljoro, Kanembwa JKT na Geita Gold Sports. Wachezaji, waamuzi, makocha
wasaidizi na baadhi ya viongozi wa ngazi za chini katika klabu hizo
wameadhibiwa kwa kupewa vifungo vikubwa.
Siku moja baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mkurugenzi wa mashindano wa
TFF akajiuzulu katika nafasi yake. Na jana ikasambaa sauti ikisikika
baadhi ya viongozi wa juu wa TFF wakipanga mipango jinsi ya kupanga
matokeo katika mechi ya Kanembwa v Geita kabla haijachezwa.
Dennis Richard golikipa wa klabu ya Simba aliye kwa mkopo Geita Gold
amefungiwa miaka kumi kujihusisha na soka huku pia akitozwa faini ya
milioni kumi.
“Mtu anayepanga matokeo Simba haimuungi mkono na inataka hatua zaidi za
kinidhamu zikichukuliwa ikithibitika. Tunasema hivi kwa sababu kuna
mchezaji wetu alikuwa kwa mkopo Geita (Dennis Richard ) amefungiwa miaka
kumi kwa tuhuma za rushwa na upangaji wa matokeo.”
“Kupanga matokeo ni kosa kubwa sana katika mpira, na mtu akibainika
afutwe si tu kufungiwa maisha. Lakini kwa tuhuma tulizozisikia jana
(kuvuja kwa sauti ya vigogo wa TFF wakipanga njama za kupanga matokeo)
tunaiomba TAKUKURU ikapige kambi TFF, pale kuna zaidi ya kilichoamuliwa
na kamati ya nidhamu.”
“Tunaiomba TAKUKURU-Mamlaka husika katika kusimamia upigaji vita rushwa
ikapige kambi pale. Uchunguzi wake uanzie juu kwani katika audio
iliyosamba jana inawataja baadhi ya viongozi wa juu wa TFF. Inaonesha
hili jambo kamati ya nidhamu ilikuwa mzigo mzito kwao,” anasema Manara. |
No comments:
Post a Comment