Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo
wa Vishale Tanzania (TADA) Bi. Subira Waziri akiongea na waandishi wa
habari hawapo pichani leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanza kwa
mashindano ya Afrika mashariki huku Tanzania ikiwa mwenyeji wa
mashindano hayo kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bi. Redempta
Mwebesa.
Waandishi wa Habari wakifuatilia
kwa makini mkutano ulioandaliwa na viongozi wa Chama cha Mchezo wa
Vishale Tanzania( TADA) hawapo pichani kuzungumzia kuhusu kuanza kwa
mashindano ya Afrika mashariki yanayotarajiwa kuanza April 29 mwaka
huu.
Mashindano ya wazi ya Kitaifa na
Kimataifa ya Shirikisho la Mchezo wa Vishale Afrika Mashariki
yanatarajiwa kufanyika April 29 mpaka Mei Mosi jijini Dar es salaam,
Tanzania ikiwa kama mwenyeji wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa
kujumuisha nchi za ukanda wa Afrika mashariki zikiwemo Tanzania kama
mwenyeji, Kenya, Uganda, Burundi na Ruanda huku Kenya ikiwa bingwa
mtetezi wa michuano hiyo.
Akizungumza hayo leo jijini Dar
es salaam Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Vishale Tanzania (TADA) Bi.
Subira Waziri amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi
zitakazoshiriki michuano hiyo ikiwa na mategemeo makubwa ya ushindi.
“Tuna matarajio ya kuibuka
washindi katika michuano hiyo kutokana na kujiandaa vya kutosha kwa
upande wa mazoezi ukizingatia kuwa tuna utayari na uzoefu wa mchezo huo”
alisema Bi. Waziri.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti
wa TADA Bi. Redempta Mwebesi amesema kuwa licha ya mashindano hayo
kuanza mwezi huu pia wana ukosefu wa Vifaa vya Michezo pamoja na gharama
za kuweka kambi ili kujifua zaidi.
Aidha Bi. Mwebesi ameongeza kuwa
wana ukosefu wa pesa taslimu na vikombe vya kuwapa washindi kwa kuwa
wanategemea viingilio kutoka kwa washiriki wa mashindano hayo.
“Tunaomba wadhamini na wadau wa
michezo wajitokeze kutusaidia kudhamini michuano hii kwa kutupa vifaa
na gharama za kukaa kambini ili tuweze kujifua zaidi na kurudisha
heshima tuliyoipata mwaka 2014 kwa kuibuka washindi wa michuano hii”
aliongeza Bi. Mwebesa.
Pia Bi. Mwebesa ameongeza kuwa
wana mikakati ya kuanzisha na kukuza mchezo huo kuanzia mashuleni ,
vijijini na Tanzania kwa ujumla ili kuweza kupanua na kuongeza ushindani
wa mchezo huo nchini.
No comments:
Post a Comment