DAR ES SALAAM: Kufuatia tabia ya akina dada wengi kuweka picha za nusu
utupu katika akaunti zao kwenye mitandao ya kijamii, wakiwemo mastaa
kama Lulu, Masogange na wengineo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imewapa kibano kikali, Risasi Mchanganyiko lina stori kamili.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Meneja
Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungi alisema ingawa jukumu la
kuwakamata wote wanaoweka picha zinazokiuka maadili ni la jeshi la
polisi kupitia kitengo cha makosa ya mtandao (Cyber Crime), taasisi hiyo
inawasiliana na wamiliki wa mitandao ya kijamii ili kutafuta namna
nzuri ya kuwadhibiti.
“Tunachofanya ni kuzungumza na hawa watu ili kuwafungia wote wanaokiuka
maadili, tunajua baadhi yao wanajiunga katika mitandao kwa kutumia
majina ya uongo, lakini sisi tutazifungia ‘line’ maana kila moja ina
namba zake za siri na hazifanani na zingine, hivyo ukiondolewa kwa
kufungiwa huwezi tena kujiunga kwa vile kule kwenye mitandao wanatambua
namba,” alisema.
Akifafanua, Mungi alisema wakifikia makubaliano na mitandao hiyo ya
kijamii aliyoitaja kuwa ni pamoja na Twitter, Facebook, Instagram,
Badoo, Snapchat na mingineyo, mtu anayeweka picha zinazokiuka maadili
atafungiwa na hataweza kujiunga tena hata abadili jina mara ngapi.
Katika mitandao hiyo, baadhi ya wasichana wakiwemo maarufu, wamekuwa
wakiweka picha zinazokiuka maadili, kwa sababu mbalimbali wengine
wakitajwa kuwa wanajiuza.
Baadhi wa wasichana wenye majina maarufu ambao wamekuwa wakitupia picha
zenye utata mara kwa mara katika mitandao licha ya Lulu ni pamoja na
Agnes Gerald ‘Masogange’, Gigy Money, Shilole, Kidoa, Anti Lulu, Isabela
Mpanda na wengineo.
No comments:
Post a Comment