Ikiwa
siku mbili baada ya Marekani kuitoa Tanzania kwenye nchi wanachama wa
Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), hivyo kukosa zaidi ya Sh.
trilioni moja, wahisani wengine 10 kati ya 14 waliokuwa wakichangia
bajeti ya serikali kuu wamejitoa. Kutokana na kujitoa huko,
Tanzania iko nja panda katia kupata Sh. Trilioni 1.37 zilizotarajiwa
kupatikana kupitia wahisani hao katika bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo
ni ya kwanza kwa serikali ya Rais Dk. John Magufuli. Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile, alisema
jijini Dar es Salaam jana kuwa wahisani wa maendeleo waliobaki kwa sasa
ni Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya (EU), Denmark na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB). Wahisani wengine waliokuwa wakisaidia bajeti
kuu ya serikali ni Uingereza, Canada, Denmark, Finland, Germany,
Ireland, Japan, Norway na Sweden. Wakati Dk. Likwalile akitaja
wahisani hao wanne waliobaki, huenda wengi zaidi wakajitoa kutokana na
tamko la mabalozi na wawakilishi wa nchi zao kuhusu uchaguzi wa
Zanzibar, ambao ndio ulifanya Tanzania ikose fedha za MCC. Nchi
hizo ni Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa,
Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi,
Uingereza na Marekani. Sehemu ya tamko la mabalozi hao
lilisema: “Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, bila
kuwepo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa
mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande
husika. “Ili uwe wa kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu. Tunarejea
wito wetu kwa serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika
suala la Zanzibar na kujielekeza katika kupatikana kwa ufumbuzi wa
mgogoro huu kupitia mazungumzo baina ya pande husika kwa lengo la
kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Katika
mkutano wa Bunge uliopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip
Mpango, aliwasilisha bungeni mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya
serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, ambao ulionyesha takribani Sh 1.37
trilioni za maendeleo zitatokana na wahisani. Mpango huo
ulionyesha sura ya bajeti ijayo itakuwa Sh. trilioni 22.99. kwa upande
wa matumizi, Sh. trilioni 16.80 ni matumizi ya kawaida na Sh. trilioni
6.65 kwa ajili ya mishahara. “Aidha, matumizi ya maendeleo
yatakuwa Sh. bilioni 6.182 na Sh. bilioni 4.81 ni fedha za ndani sawa na
asilimia 77.8 ya fedha za maendeleo,” alisema. Akizungumza
na waandishi wa habari jana baada ya kusainiana mkataba wa makubaliano
baina ya serikali ya Japani na Tanzani kwa ajili ya kupatiwa Sh. bilioni
116.4 za kuisaidia bajeti ya 2015/16, Dk. Likwalile alisema kujitoa kwa
wahisani hao kumesababishwa na changamoto kwenye nchi zao. Wakati
akisema hayo, tangu mwaka juzi wahisani wengi walianza kusuasua
kuchangia bajeti ya serikali kutokana na kashfa za rushwa, ikiwamo ile
ya kuchotwa kwa Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Dk Likwalile alisema mchango wa
wahisani katika bajeti ya 2014/2015 ilikuwa Sh. trilioni moja na katika
bajeti iliyofuata ilishuka hadi Sh. bilioni 800 kwa bajeti ya 2015/2016
na hadi sasa wamechangia Sh. bilioni 400. Alisema licha ya
wahisani hao kujitoa kuchangia bajeti ya serikali, wamechangia moja kwa
moja kupitia kwenye miradi mbalimbali. Dk. Likwelile alisema bado
wana mazungumzo na washirika wa maendeleo hivyo orodha inaweza
kuongezeka kwa kuwa wamejipanga katika mfumo mzuri wa fedha. Alisema
wamechukua wataalamu elekezi kuangalia mfumo mzima wa ushirikiano na
kwamba katika mwaka mwingine wa fedha kutakuwa na mabadiliko. Pia
alisema kuna uboreshwaji mkubwa uliofanywa na serikali iliyopo
madarakani hasa katika matumizi ya fedha pamoja na ukusanyaji wa mapato
ambapo tayari wahisani hao wameona kazi nzuri inayofanywa. “Tunaendelea
vizuri na mazungumzo kujitoa kwao katika kuchangia bajeti ya serikali
siyo kwamba hawatusaidii bado wanaendelea kufadhili baadhi ya miradi
moja kwa moja,” alisema Dk. Likwelile Alipohojiwa ni madhara
gani yanaweza kutokea kwa kukosekana fedha za MCC katika kuendeleza
miradi ya umeme vijijini, Dk. Likwelile Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
haiwezi kuathirika kwa vile fedha hizo ambazo ni dola milioni 472
hawakuziweka kwenye bajeti. Alisema fedha hizo zilikuwa kwa
ajili ya kuboresha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la
Umeme Zanzibar (ZECO), miundombinu ya umeme na kuwawezesha wafanyabiasha
kupata vifaa vya umeme. Kuhusu makubaliano waliyoingia baina
ya serikali ya Japani na Tanzania, alisema fedha hizo kwa ajili ya
kuisaidia bajeti ya serikali pamoja na kuboresha biashara kwa lengo la
kuongeza ajira. Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini
Tanzania, Masaharu Yoshida, alisema mradi huo ni wa kwanza kati ya
mitatu ya uendeshaji wa sera za maendeleo na kupitia mradi huu, wataunga
mkono juhudi za Tanzania za kuongeza fursa za uzalishaji wa ajira, hasa
kwenye sekta binafsi kwa kupunguza gharama za kufanya biashara. Yoshinda
alisema wanaelewa msingi wa kuimarisha utendaji kwenye sekta binafsi na
kukuza uzalishaji wa ajira ni muhimu kwa maendeleo zaidi ya Tanzania. Wakati
huo huo, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), ambaye ni Waziri Kivuli wa
Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Mchungaji Peter Msigwa, ametoa tamko zito baada ya Tanzania kuenguliwa
katika misaada ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC). Katika
tamko hilo, Msigwa ameutaka Umoja wa Ulaya (EU) nayo kuzuia misaada
kwa serikali ya Tanzania kutokana na mwenendo wake katika uopngozi wa
nchi hususan demokrasia. Akizungumza jana mjini hapa, Msigwa
alisema kambi ya upinzani imesikitishwa na maelezo ya Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk.
Augustino Mahiga, kutowaeleza wazi Watanzania sababu hasa ya serikali
ya Marekani kusitisha utolewaji wa fedha hizo za msaada, badala yake
kueleza mambo yasiyo na mashiko. Alisema MCC ilieleza maeneo
ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi wa Zanzibar
na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mtandaoni, inayonyima
uhuru wa wa kujieleza na uhuru wa kujumuika. Mchungaji Msigwa
alisema kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa kushtushwa
na uamuzi wa MCC kwa kuwa serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo
vya kustahili kupewa misaada na MCC. Alsiema inashangaza na
kusikitisha kuona Balozi Mahiga, msomi na mwanadiplomasia mzoefu kama
akilitia taifa aibu ya mwaka kwa kulalamikia kuonewa. “Kauli
ya Waziri Mahiga za kukataa kukiri makosa yaliyo dhahiri yaliyofanywa na
serikali ya CCM zinaweza kabisa kuuweka rehani uhusiano na ushirikiano
mzuri wa kidiplomasia ambao Tanzania imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi
mbalimbali na mashirika ya kimataifa kama MCC. “Tukiweka
mbele maslahi ya nchi hii yakiwamo ya kudumisha uhusiano wa kimaendeleo
na nchi zingine, Kambi rasmi ya Upinzani tunaiomba MCC, Marekani na
mataifa mengine kuzipuuza kauli zilizotolewa na Waziri Mahiga, kwani
haziakisi ustaarabu wa Watanzania,” alisema Msigwa. Pia
alisema Tanzania si mbia mgeni kwa MCC kwakuwa ilishapokea awamu ya
kwanza ya fedha za msaada za dola za milioni 698. Fedha hizo zilitumika
kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro
na Namtumbo - Songea hadi Mbinga. Aidha, alisema kuwa fedha
hizo zilitumika pia kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya
miji ya Dar es Salaam na Morogoro na kusambaza umeme katika vijiji vya
mikoa 10 ya Tanzania Bara pamoja na kutandaza njia ya pili ya
kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania
Visiwani na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya
barabara za Unguja kwa kiwango cha lami. |
No comments:
Post a Comment