Baadhi ya wataalamu na waandishi wa habari mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es salaam. |
Baadhi ya wataalamu namaofisa kutoka taasisi mbalimbali wakiwa katika uzinduzi huo.
Utafiti mpya Watoa Makadirio ya Kwanza Kitaifa ya Matukio ya Utoaji Mimba Nchini
Katika utafiti wakilishi wa
kwanza kitaifa kuhusu matukio ya utoaji mimba na huduma baada ya
kuharibika kwa mimba nchini Tanzania, watafiti waligundua kwamba utoaji
mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye
vifo na kuumia kwa wajawazito. Utafiti huo, uliofanywa na watafiti kutoka taasisi ya Guttmacher iliyoko Marekani, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
zilizoko hapa Tanzania, waligundua ya kwamba makadirio ya mimba 405,000
zilitolewa nchini ndani ya mwaka 2013, nyingi zikitolewa kwa taratibu
ambazo si salama na kuhatarisha maisha ya wanawake. Kutokana na
mchanganyiko wa sheria tata na yenye vizuizi vingi ya utoaji mimba ya
Tanzania, wanawake hutafuta huduma za utoaji mimba zinazofanyika kisiri
na ambazo si salama.
Watafiti hao, ambao walifanya
utafiti kwenye vituo vya afya, miongoni mwa wataalamu wa afya na kufanya
mapitio ya taarifa za idadi ya watu na uzazi, wamekadiria kwamba
wanawake 66,600 walipewa huduma baada ya kuharibika kwa mimba kwenye
vituo vya afya kutokana na matatizo yaliyotokana na utoaji mimba usio
salama ndani ya mwaka 2013. Hata hivyo, karibu wanawake 100,000 ambao
walipata matatizo hawakupata matibabu ambayo waliyahitaji. Watafiti
wanatumaini kwamba matokeo yao yatasaidia kutaarifu juhudi
zinazoendelea nchini Tanzania kupunguza uwiano wa vifo vya wajawazito,
ambao umebaki kuwa miongoni mwa iliyo juu zaidi duniani.
“Kwa kutambua kuwa utoaji mimba
usiokuwa salama ni chanzo kikuu cha vifo vya wajawazito, Serikali ya
Tanzania imepanua wigo wa upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa
mimba katika muongo mmoja uliopita, lakini mapungufu makubwa bado yapo
na wanawake wengi hawapati huduma wanazohitaji,” alisema Sarah C. Keogh,
mtafiti mwanasayansi mwandamizi wa taasisi ya Guttmacher na mwandishi
kiongozi wa utafiti huo. “Utafiti huu unabainisha mapungufu hayo na
kusaidia kuunda mikakati kuhakikisha kuwa kila mwanamke wa Kitanzania
anayehitaji anaweza kupata huduma baada ya kuharibika kwa mimba
inayoweza kuokoa uhai.”
Kiwango cha kitaifa cha utoaji
mimba nchini Tanzania—36 kwa kila wanawake 1,000 walio kwenye umri wa
uzazi—kinafanana na viwango vya nchi nyingine za Afrika Mashariki. Hata
hivyo, ndani ya Tanzania viwango vya utoaji mimba vinatofautiana kwa
ukanda. Viwango vya juu ya utoaji mimba hupatikana katika Kanda ya Ziwa
(51 kwa kila wanawake 1,000) na Nyanda za Juu Kusini (47 kwa kila
wanawake 1,000), na kiwango cha chini hupatikana Zanzibar (11 kwa kila
wanawake 1,000). Viwango hivi tofauti vya utoaji mimba huhusishwa
kimsingi na utofauti katika viwango vya matumizi ya njia za uzazi wa
mpango na mimba zisizotarajiwa, na uwezekano wa wanawake kuamua kutoa
mimba katika tukio la kupata mimba zisizotarajiwa.
“Mbali na huduma baada ya
kuharibika kwa mimba, wanawake wa Kitanzania wanahitaji upatikanaji bora
na kamilifu wa huduma mbalimbali za njia za uzazi wa mpango na ushauri
nasaha kuhusu uzazi wa mpango ili waweze kufanya maamuzi sahihi,”
alisema Godfather Kimaro,
mwanasayansi mtafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu nchini Tanzania, ambaye alifanya kazi kwenye utafiti. “Ndani ya
mwaka 2013, wanawake wa Kitanzania walipata mimba zisizotarajiwa zaidi
ya milioni moja, ambazo kati yake 39% ziliishia kwenye kutolewa.
Kukabiliana na mahitaji yasiyokidhiwa ya uzazi wa mpango kutapunguza
kiwango cha mimba zisizotarajiwa na hivyo kupunguza uhitaji wa kutoa
mimba na vifo na majeruhi ambayo kwa mara nyingi hutokea baada ya
taratibu zisizo salama.”
Watafiti wamependekeza kuimarisha
juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa
mimba, ambayo kwa sasa inapatikana bila ulinganifu katika maeneo
mbalimbali. Wamependekeza uwekezaji katika kufanya huduma baada ya
kuharibika kwa mimba inapatikana katika ngazi zote za mfumo wa afya,
ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo watoa huduma wa ngazi ya kati na
kusambaza kikamilifu dawa na vifaa vyote muhimu kwenye vituo vya afya.
Pia, walisisitiza umuhimu wa kujumuisha utoaji wa huduma za uzazi wa
mpango kama sehemu ya huduma baada ya kuharibika kwa mimba na kuhimiza
kwamba kila mwanamke anayetibiwa kutokana na matatizo yanayohusiana na
kutoka kwa mimba apewe ushauri wa kina na nyenzo za uzazi wa mpango.
Hatimaye, walipendekeza kwamba utata katika sheria ya utoaji mimba ya
Tanzania ufafanuliwe kuhakikisha kuwa wanawake wanaweza kupata utaratibu
salama na wa kisheria kwa kiasi kamili kinachoruhusiwa. Watafiti
wanatumaini kwamba matokeo ya utafiti huu yatasaidia kuleta mwanga
kwenye sera na mipango ambayo italeta huduma za kifanisi zaidi na
hatimaye kuboresha hali ya afya ya uzazi ya wanawake wote wa Tanzania.
“Matukio ya Utoaji Mimba na Huduma Baada ya Kuharibika kwa Mimba Nchini Tanzania” na Sarah C. Keogh wa Taasisi ya Guttmacher et al. inapatikana mtandaoni kupitia PLoSONE.
Utafiti huu uliweza kufanyika
kutokana na misaada kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, Idara ya
Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, na Shirika la
Ushirikiano wa Maendeleo la Norway |
No comments:
Post a Comment