Thursday, 31 March 2016

Uchunguzi wa kusafirisha tumbili wakamilika.



Kikosi kazi maalumu cha kuchunguza makosa ya kihalifu kimekamilisha uchunguzi wa tuhuma za usafirishaji Tumbili 61
zinazowakabili raia wawili wa Uholanzi na Watanzania wawili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alilithibitishia gazeti hili jana kukamilika kwa uchunguzi huo na kusema jalada limepelekwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.

Kauli ya Mutafungwa imekuja wakati kuna uvumi uliozagaa kuwa watuhumiwa hao wataachiwa huru wakati wowote kuanzia jana bila kufunguliwa mashtaka.

Kamanda Mutafungwa alisema kuwa wao kama chombo cha uchunguzi, wametimiza wajibu wao na mwenye uamuzi wa kushtaki au kutoshtaki ni Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) baada ya kupitia ushahidi.

Hata hivyo, alisema kuwa watuhumiwa hao wanne bado wanashikiliwa na polisi wakisubiri maelekezo ya kisheria ya DPP, hivyo siyo sahihi watu kuvumisha kuwa wameachiwa bila masharti.

Watuhumiwa hao ni Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Dk Charles Mulokozi na Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Utalii wa Picha na Sites cha jijini Arusha, Nyangabo Musika. Watuhumiwa wengine ni raia hao wa Uholanzi ambao ni ndugu wa familia moja, Artem Alik Vardanyian (52) na Eduard Alik Vardanyian (44).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipoulizwa juzi kuhusu uvumi wa kutoshtakiwa kwa watuhumiwa, alisema yeye ametimiza wajibu wake. 

No comments: