Maafisa watatu
wamefikishwa kortini Dar es Salaam leo wakishtakiwa kuhusiana na kashfa
ya udanganyifu wa riba ya mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 600 ambazo
zilikopwa na serikali ya Tanzania kutoka kwa benki ya Standard ya
Uingereza.
Walioshtakiwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato nchini Tanzania na Mwenyekiti wa ‘Enterprise Growth Market
Advisors Ltd’ (EGMA), Bw Harry Kitilya, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya
Ushirikiano na Uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare
pamoja na aliyekuwa Mwanasheria wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bw Sioi
Graham Solomon.
Pamoja na makosa mengine, washtakiwa wote
wameshtakiwa kwa makosa ya kula njama na kujipatia fedha kwa
udanganyifu, kughushi nyaraka na utakatishaji wa fedha haramu kinyume na
sheria.
Wote wamekana mashtaka hayo.
Washtakiwa wote watatu wamepelekwa rumande baada ya kukosa dhamana na kesi hii itatajwa tena tarehe 8 Aprili 2016.
Kashfa
hii ilitokana na kitendo cha Benki ya Standard kukubali kuipokesha
Serikali ya Tanzania kiasi cha Dola milioni 600 mwaka 2012 kwa masharti
ya kulipwa riba ya asilimia 1.4.
Lakini Benki ya Stanbic, tawi la
Tanzania iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya serikali kutakiwa
kulipa riba ya asilimia 2.4. |
No comments:
Post a Comment