Rais wa Afrika
Kusini Jacob Zuma amekubali uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba uliompata na
hatia kuhusiana na ukarabati uliofanywa katika makao yake ya kibinafsi
eneo la Nkandla.
Akihutubia taifa hilo moja kwa moja kupitia
runinga, Bw Zuma amesifu mahakama hiyo na kusema imedhihirisha kuwepo
kwa uhuru wa mahakama nchini humo.
Amesema uamuzi wa mahakama hiyo
ni wa kihistoria kuhusu uamuzi wa mkaguzi wa hesabu za umma
aliyewasilisha kesi dhidi yake mahakamani.
"Mahakama imeamua
kwamba uamuzi wa mkaguzi wa hesabu za umma ni wa mwisho na anayetaka
kubadili hilo lazima apitie kwa mahakama," amesema Bw Zuma.
Kiongozi huyo amesema atakubali kulipia ukarabati uliofanyiwa makao hayo ya Nkandla kama ilivyoamua mahakama.
"Nimekuwa
nikisisitiza kwamba niko tayari kulipia ukarabati usiohusiana na
usalama katika mahakama yangu, taasisi rasmi ikifanya hesabu hiyo na
kutoa uamuzi," amesema.
Bw Zuma amesema pia kwamba anakubali kwamba hatua yake ya kukosa
kutii uamuzi wa mkaguzi wa hesabu za umma ni makosa na ukiukaji wa
katiba.
Hata hivyo amesisitiza kwamba hakufanya hivyo makusudi.
"Awali,
nilifuata njia tofauti ambayo ni sahihi kisheria wakati huo, lakini
baadaye imebainishwa kuwa kinyume cha katiba. Kama Mahakama ya Kikatiba
ilivyosema, nilifuata njia tofauti nikifuata uamuzi wa Mahakama ya Juu
ya Western Cape. Uamuzi huu baadaye ulibatilishwa baada ya rufaa na mara
moja nilianza kufuata uamuzi wa Mahakama ya Rufaa," amesema.
"Nia
yangu haikuwa kutaka kujinufaisha kupitia ufisadi au kutumia mali ya
umma kujifaidi au kufaidi familia yangu. Hivyo, nimeamua kulipia gharama
ya vitu vinavyotakikana utathmini ukifanywa."
Amesema kuna mafunzo ya maafisa wa serikali kujifunza kwa ajili ya siku za usoni.
Ameeleza
kuwa mradi huo wa Nkandla umefichua udhaifu wa mfumo wa ununuzi wa mali
ya umma. Amekiri kwamba gharama ya ukarabati wa makao yake iliongezwa
sana jambo ambalo halikufaa kufanyika. |
No comments:
Post a Comment