Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali zaMitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. George
Simbachawene amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanakusanya mapato
vizuri kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato na
kutumia vizuri fedha zilizokusanywa ili kuwaletea maendeleo wananchi
katika mikoa yao.
Akizungumza katika kikao kati yake
na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa cha kujadili mwelekeo wa
bajeti za Mikoa na Halmashauri iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee
jijini Dar es Salaam hivi karibuni Mhe. Simbachawene aliwataka Wakuu wa
Mikoa kutumia umahiri na ustadi zaidi katika kubuni vyanzo vipya vyama
pato zaidi ya vile vilivyozoeleka kila siku ili kupata fedha za
kutekeleza shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Mipango ya bajeti zetu lazima
zinakisi matatizo yaliyopo, hakikisheni rasilimali chache zinazopatikana
zinatumika vizuri na pia hakikisheni Kuwa kila fedha inayopatika na
inawekezwa katika eneo husika na kwa kufanya hivyo maendeleo
yataonekana”. Alisema Mhe. Waziri
Mhe. Simbachawene aliwataka Wakuu
wa Mikoa kuwatumia Wakuu wa Wilaya katika maeneo yao kutatua kero na
migogoro ya wananchi kwani alisema kwa kufanya hivyo itaepusha wananchi
kufikisha malalamiko yao ngazi za juu kwa kuwa tayari matatizo yao
yatakuwa yameshughulikiwa katika ngazi za chini.
“Migogoro mingi inayowasilishwa na
wananchi inahusu dhuluma, migogoro ya ardhi na kutotendewa haki kwa
wananchi. Ukiona wananchi wanakuja juu kuleta malalamiko ujue huko
chini hawakushughulikiwa vizuri. Jaribuni kumaliza matatizo ya wananchi
huko chini na kuwafanya wananchi kuishi kwa amani na furaha”.
Alisisitiza Mhe. Simbachawene
Waziri wa Nchi pia aliwataka Wakuu
wa Mikoa kukuza ajira katika maeneo yao kwa kuanzisha viwanda vidogo na
vya kati ili kuwaletea vijana ajira na kuisaidia serikali kufikia lengo
lake la kuwa nchi yenye uchumi wa kati baada ya kila Mkuu wa Mkoa
kutafsiri matarajio ya Serikali Kuu kwa vitendo.
“Anza kutekeleza malengo kwa
kuangalia dira ya serikali ya kuifanya nchi yetu kufikia uchumi wa kati
na wakati unapoanza kutekeleza mapema anza kuona kama kuna vikwazo vya
kufikia lengo na kuliwasilisha sehemu husika ili serikali ione namna ya
kukusaidia kufikia lengo. Alieleza Mhe. Simbachawene.
Aidha, aliwaagiza Wakuu wa Mikoa
kuhakikisha wanasimamia vizuri suala la utoaji wa Elimu Msingi bila
malipo pamoja na kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa hazizalishi
madeni na hivyo kutoruhusu madeni kuongezeka.
Katika kikao hicho Wakuu wa Mikoa
pia waliwasilisha kwa Waziri wa Nchi-TAMISEMI taarifa za zoezi la
uhakiki wa watumishi hewa katika mikoa yao ambapo Mhe. Waziri
Simbachawene alizipokea na alieleza kuwa ataziwasilisha kwa Waziri wa
Utumishi kwa ajili ya kuziweka vizuri na baadaye zitawasilishwa kwa Mhe.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
No comments:
Post a Comment