Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani ambaye
amekuwa akiongoza kwenye kinyang’anyiro hicho, Donald Trump amejikuta
akikosolewa vikali kuhusu upeo wake juu ya sera za nje pale aliposhindwa
kulitamka bayana jina la Tanzania.
Drump ambaye Jumanne aliyopita alivuna ushindi wa kishindo kwenye
majimbo yote manne yaliyopiga kura za mchujo alijikuta akitumbukia
kwenye kadhia hiyo wakati akielezea vipaumbele vya Marekani kuelekea
mataifa ya kigeni.
Alikuwa akigusia juu ya mashambulizi ya mabomu yaliyotokea katika
ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya na kusababisha uharibifu
mkubwa wa mali huku watu kadhaa wakipoteza maisha.
Akiwa katika hali ya kujiamini, Trump alisema kuwa iwapo ataingia
madarakani moja ya vipaumbele vyake ni kuendelea kutetea masilahi ya
Marekani na kudhihirisha hilo aliamua kutolea mfano mashambulizi hayo ya
kigaidi.
Lakini wakati akilitaja jina la Tanzania, mfanyabiashara huyo alijikuta
akigusa hisia za wengi pale alipolitaja jina hilo kinyume na
inavyotamkwa. “ Ona mashambulizi yaliyotokea katika miaka ya 1990 katika
ubalozi wetu nchini Tan-ZAY-nee-uh”.
Matamshi hayo yalizusha mjadala mkubwa huku baadhi ya wakosoaji wake
wakiingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kumuelezea kama ni mtu
asiyekuwa na upeo mkubwa kuhusu siasa za kimataifa.
Baadae kambi ya kampeni ya Trump ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari
ikisema kuwa kuteleza kwa mgombea wao katika matamshi ya jina halisi la
Tanzania hakumaanishi kuwa uwezo wake kuhusu masuala ya
usalama,diplomasia ya kimataifa na biashara ya kimataifa ni wa kutiliwa
mashaka.
No comments:
Post a Comment