Mheshimiwa
Spika, Tangu tuanze Mkutano huu wa Bajeti mwaka 2016 kumekuwa na
malalamiko kutoka kwa Wabunge na hasa wabunge wa kambi ya Upinzani
Bungeni kuhusu ukiukwaji wa Sheria mbalimbali za nchi katika masuala ya
Bajeti.
Jana
jioni Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Andrew Chenge alitoa Changamoto
kuwa Wabunge tuseme ni sharia gani zimekiukwa katika mchakato mzima wa
Bajeti ya Nchi hivi sasa. Kwa maoni yangu, kuna ukiukwaji kadhaa wa
sharia ya Bajeti, sharia namba 11 ya mwaka 2015 katika mchakato wa
Bajeti ya Mwaka huu. Nitaeleza kwa ufupi.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8 cha sheria ya Bajeti kinaeleza namna ambavyo mfumo wa Bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.
Vifungu
cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa Bajeti
unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka “Planning and Budget Guidelines”
zipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Mwezi Februari kila mwaka.
Sheria inataka “budget ceilings” ziidhinishwe na Kamati ya Bajeti na
baadaye Bunge linapokaa kama Kamati ya Mipango.
Mheshimiwa
Spika, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa
Bajeti uliokuwa na Bajeti ya Tshs 23.7 trilioni kama ulivyowasilishwa na
Waziri wa Fedha na Mipango. Hata hivyo Bajeti inayojadiliwa sasa ni
Tshs 29.5 trilioni tofauti kabisa na sio tu viwango vilivyopitishwa na
Bunge mwezi Februari bali pia hata vipaumbele vyake ni tofauti.
Hili
ni suala la Utawala bora (governance issue) kwani taratibu za utungaji
wa Bajeti zimeainishwa na sheria na kama sheria hazifuatwi ni vigumu
sana hata Bajeti yenyewe kutekelezwa.
Ili
kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama kamati ya Mipango
na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa Bajeti
kuendelea au angalau kabla ya kupitisha Bajeti Kuu mwezi wa Juni 2016.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Rais Ikulu inapasa kuzingatia sana sheria na taratibu
tulizojiwekea kwani madhara ya kutofuata sheria ni makubwa mno.
Kwa
mfano hivi sasa Bajeti za Taasisi hazimo kwenye vitabu vya Bajeti ya
Serikali kinyume na Sheria ya Bajeti ambapo hivi sasa Bajeti za Taasisi
zote za Umma zinakuwa ni sehemu ya Bajeti ya Serikali na Wabunge
wanapaswa kuwa na nyaraka za bajeti hizo.
Ofisi
ya TR kwa mujibu wa kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti ilipaswa
kuunganisha Bajeti za Mashirika yote ya Umma na kutoa kitabu chake kwa
Wabunge.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa Wabunge kuhusu
masuala haya ili kuzuia ukiukwaji wa Sheria tulizojitungia wenyewe.
TAKUKURU na kesi za Ufisadi Mkubwa Nchini
1. Ufisadi wa HatiFungani ya Tshs 1.2 trilioni Standard Bank ya Uingereza
Mheshimiwa
Spika, Tarehe 8 Machi mwaka 2013 Serikali ya Tanzania ilikopa fedha
$600 milioni ( 1.2 trilioni) kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard
ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc. Mkopo huo wenye
riba yenye kuweza kupanda (floating rate) umeanza kulipwa mwezi Machi
mwaka huu ( kama Serikali imeanza kutekeleza mkataba).
Mkopo
huu utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo 9 inayolingana. Ifikapo mwaka
2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba jumla ya $897 milioni (
takribani tshs 2 trilioni ).
Mkopo
huu umegubikwa na ufisadi na kwa kuwa baadhi ya Watanzania wamefikishwa
mahakamani kuhusiana na sehemu ya mkopo huu, sitapenda kueleza upande
wa waliopo mahakamani.
Kesi
iliyopo mahakamani inahusu $6 milioni ambazo inasemekana ( kwa mujibu
wa nyaraka za mahakama) kuwa zilitumika kuhonga maafisa wa Serikali ili
Benki hiyo ya Uingereza iweze kupata biashara iliyopata.
Jambo
la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo
mahakamani mpaka sasa. Vile vile waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani
mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekena kutumika kupeleka
rushwa.
Mjumbe
kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa
kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua
Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.
Mheshimiwa
Spika, Hapa mbele yangu nina barua ambayo kundi la Watanzania zaidi ya
2000 kutoka kona zote za dunia wamesaini kutaka Benki ya Standard ya
Uingereza ichunguzwe kwenye suala hili la HatiFungani.
TAKUKURU
walitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya SFO katika kuchukua hatua
zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hili.
SFO
haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard Bank.
Hatujui ni kwa maslahi mapana ya Uingereza au ni kwa kupitiwa. Sisi
Tanzania tumejikuta tunafuata matakwa ya Uingereza katika jambo hili,
kiasi cha hata kutumia ushauri wa kitaalamu wa Waingereza katika jambo
hili.
Leo
hii TAKUKURU inasaidiwa katika kesi hii na wataalamu kutoka Uingereza
katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza! Watanzania walioandika
petition kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote
kujulikana – Standard Bank walihusika kwa kiwango gani katika kutoa
rushwa ili kupata biashara? TAKUKURU wanapaswa kufanyia kazi jambo hili
kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, mashtaka ya kutoa rushwa ili
kupata biashara nchini.
Hata hivyo TAKUKURU inaogopa wazungu, inaogopa kuwaudhi watu wanaowapa ushauri wa kitaalamu kuhusu kesi za rushwa!
Mheshimiwa
Spika, maslahi ya Tanzania hapa ni makubwa mno. Iwapo tutafanikiwa
kuonyesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu
Tanzania itafaidika kwa namna mbili.
Moja,
itakuwa ni fundisho kubwa kwa makampuni ya kimataifa kwamba Afrika sio
mahala pa kuhonga na kupata kazi na kutoadhibiwa. Mbili, Tanzania
haitalipa mkopo huu na riba zake.
Tutakuwa
tumeokoa zaidi ya tshs 2 trilioni katika Deni la Taifa na kuelekeza
fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi wetu
kwenye Afya na Elimu.
TAKUKURU
waongozwe na maslahi mapana kwa Taifa badala ya kutafuta sifa ndogo
ndogo za ‘wangapi wamefikishwa mahakamani’. Ni lazima taasisi zetu sasa
zianze kutazama mambo kwa picha kubwa.
Mheshimiwa
Spika, hii sio mara ya kwanza SFO kufanya ilichofanya dhidi ya
Tanzania. Mnakumbuka kesi ya rada na Shirika la BAE la Uingereza. Safari
hii Tanzania isikubali kubeba tu makubaliano ambayo SFO inafanya na
makampuni ya kimataifa.
Ni
lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya.
Haiwezekani wawe ni Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha
wanaotoa rushwa hizo wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Mheshimiwa
Spika, Taarifa zilizopo sasa kwenye vyombo vya habari ni kwamba Benki
hii kupitia tawi lake la Tanzania ( Stanbic Bank ) siku ambayo walipata
‘deal’ la Bond ndio siku hiyo hiyo walipewa kazi na Serikali ya kufungua
akaunti ya Escrow kuhusu fedha za Bomba la Gesi kutoka Mtwara.
Kimsingi
biashara hii ya Escrow akaunti katika Benki hii ni kubwa zaidi kutoka
ile ya mkopo kwani ni biashara ya kutunza fedha za Bomba kwa miaka 20!
Benki hii ilipata biashara kubwa kama hii bila ya kuwepo kwa zabuni
yeyote ile na kuleta ushindani.
Lakini
pia kama kulikuwa na umuhimu wa kufungua akaunti hii ni kwanini Shirika
la TPDC halikufungua akaunti hii katika Benki Kuu ya Tanzania? Haya
ndio mambo TAKUKURU wanapaswa kuchunguza katika kulinda maslahi ya nchi
yetu dhidi ya makampuni makubwa kutoka nje.
Mheshimiwa
Spika, Vile vile kuna taarifa kwamba hata fedha ambazo zilipatikana
kutokana na mkopo huu hazikufika kule kunakotakiwa.
Nimewasilisha
maswali Wizara ya Fedha kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi
zilikwenda. Hata hivyo kutokana na orodha ya miradi niliyonayo na
kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na wakandarasi,
mradi wa Kinyerezi na hata mradi wa Kiwira, ni dhahiri kuwa sehemu ya
fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko. Uchunguzi wa
kina unatakiwa kwenye eneo hili ili kupata ukweli na kuzuia mambo kama
haya kutokea siku za usoni.
Mheshimiwa
Spika, nitatumia kanuni ya 120(2) kutaka Bunge tako tukufu kuunda
Kamati Teule kuichunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni
yake dada ya Stanbic Tanzania kuhusiana na Mkopo wa Hatifungani $600m,
matumizi ya mkopo huo na ufunguzi wa Akaunti ya Escrow ya Bomba la Gesi
la Mtwara – Dar es Salaam.
Kwa
sasa ninawasilisha mezani nyaraka zote nilizonazo kuhusiana na Mkopo
huu kwa ajili ya Bunge kupitia kabla ya kuwasilisha Hoja ya Kuundwa kwa
Kamati Teule ya Bunge kuichunguza Standard Bank ICBC na Stanbic Tanzania
2. Uchunguzi wa IPTL Tegeta Escrow Account
Mheshimiwa
Spika, Mwaka 2014 TAKUKURU waliijulisha Kamati ya Bunge ya PAC kwamba
ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka
Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc
Tanzania.
Katika
taarifa zote ambazo TAKUKURU inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna hata
siku moja wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini wahusika waliochota
fedha za umma watafikishwa mahakamani. Naomba tupate kauli ya Serikali
kuhusu jambo hili kwani ni moja ya JIPU kubwa ambalo tunadhani Serikali
inalikimbia.
Serikali inaogopa nini? Serikali inamwogopa nani? Kwanini kesi ya ufisadi wa IPTL unakaliwa kimya? Kwa maslahi ya nani?
No comments:
Post a Comment