Serikali
imeshauriwa kuwa na sehemu ya umiliki katika kampuni zinazochimba
madini na gesi ili kujua mapato halisi yanayoingizwa na wawekezaji wa
kigeni.
Aidha,
imeshauriwa kuzilazimisha kampuni hizo kurejesha nchini asilimia 60 ya
mauzo yake, ili kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, pamoja na
kuimarisha Shilingi ya Tanzania.
Ushauri
huo ulitolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
aliyestaafu, Ludovick Utouh pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uhamasishaji wa Uwazi katika mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (EITI),
Jaji mstaafu Mark Bomani, wakati wa uzinduzi wa ripoti za kamati za
mwaka 2013 na 2014 uliofanyika jana Dar es Salaam.
Akizindua
ripoti hizo, Utouh alisema, Tanzania haijafaidika na rasilimali za
madini, jambo lililosababishwa na kujiondoa kufanya biashara, hivyo
kuzipa mwanya kampuni za kigeni kuendesha biashara bila uwazi kuhusu
mapato zinazoyapata kutokana na mauzo ya madini.
“
Serikali iliangalie jambo hili na kulirekebisha, Serikali ya Botswana
ina hisa kwenye migodi hiyo, hivyo wanakuwa na mwakilishi kwenye bodi
jambo ambalo linakuwa rahisi kufuatilia mapato yanayopatikana, lakini
sisi hapa tulijiondoa kwa madai kuwa Serikali haifanyi tena biashara,” alisema Utouh.
Alisema,
Serikali ikifanya hivyo itaweza kupata mapato mengi zaidi kuliko ilivyo
sasa, ambapo imejiondoa kabisa katika umiliki wa migodi ilhali
rasilimali hizo ni za Watanzania.
“Wawekezaji
wanakuja na fedha na utaalamu, lakini sisi cha kwetu ni rasilimali, ni
lazima tugawane nao na tuwe na mwakilishi kwenye bodi, badala ya
kusubiri mrabaha unaotokana na faida anayopata mwekezaji. Huu utaratibu
wa kuwaachia kila kitu sio mzuri,” alisema Utouh.
Naye
Jaji Bomani alisema, Serikali inatakiwa kuzilazimisha kampuni
zinazochimba madini nchini kurejesha asilimia 60 ya mauzo yake ili
kuimarisha akiba ya fedha za kigeni. Alisema, kwa kufanya hivyo,
Shilingi ya Tanzania itaimarika.
Alisema,
hatua hiyo ikichukuliwa, sekta ya madini itakuwa imetoa mchango wake
kwa pato la Serikali, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta hiyo.
Alitaja
moja ya changamoto hizo kuwa ni kupanua wigo wa wachimba madini kama
vile wachimbaji wa kati na ambao pato lao linazidi Sh milioni 200, kwa
mwaka ambao, alisema wanastahili kutoa mchango kwa pato la Serikali.
Alisema
mpaka sasa ni kampuni kubwa tu zinahusika, lakini akasema umefika
wakati wachimbaji wa kati nao waingizwe kwenye utaratibu huo.
Alipendekeza
kuwa umefika wakati sekta ya madini ipanuliwe hadi kwenye uchimbaji wa
makaa kuiwezesha nchi kufaidika zaidi na shughuli za rasilimali hiyo,
ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
EITI
ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa mwaka 2002 na nchi mbalimbali
zenye sekta ya madini. Linafanya ufuatiliaji juu ya sekta ya madini na
gesi na kuona kama kuna uwazi katika biashara yake.
No comments:
Post a Comment