Kufanikiwa kwa juhudi za
Kutokomeza ugonjwa wa Malaria kutaufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri na
salama pa kuishi kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo na kuwawezesha
mamilioni ya watu kufikia malengo yao kimaisha.
Hivi karibuni Tanzania
imeungana na nchi nyingine Ulimwenguni kuadhimisha siku ya Malaria
duniani ambapo ni maalumu kwa ajili ya kuhamasisha umma kuhusu umuhimu
wa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika jamii.
Takwimu kutoka Shirika la Afya
ulimwenguni WHO za mwaka 2002 zinaonyesha kuwa kila mwaka watu kati ya
milioni 300 hadi 500 duniani wanapata ugonjwa wa malaria, kati yao watu
milioni moja na nusu hufariki kutokana na ugonjwa huo.
Kulingana na takwimu hizo
katika bara la Afrika watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano
ndiyo wanaathirika zaidi na ugonjwa wa malaria ambapo kila mwaka watoto
milioni tano wanakufa kwa ugonjwa huo barani Afrika.
Kwa mujibu wa WHO idadi vifo
vinavyotokana na ugonjwa wa malaria hadi kufikia mwaka 2013 vilipungua
kwa takriban asilimia 20 tu duniani kote katika muongo mmoja uliopita
ambapo theluthi moja ya nchi 108 ambazo malaria ilikuwa imeenea
zilitarajiwa kutokomeza ugonjwa huo katika kipindi cha miaka 10.
Kufuatia ufanisi mkubwa
uliopatikana chini ya malengo ya maendeleo ya milenia, ni muhimu
kuuendeleza ufanisi huu na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria chini
ya malengo ya maendeleo endelevu.
Kauli mbiu hiyo inaenda
sambamba na lengo la kuwa na ulimwengu usio na malaria lilijumuishwa
katika mkakati wa kiufundi wa kimataifa kwa ajili ya malaria 2016 hadi
2030, ulioidhinishwa Mei mwaka uliopita na baraza kuu la Afya duniani.
Mkakati huo unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya malaria
ulimwenguni katika kipindi cha miaka 15 ijayo.
Kwa mujibu wa ripoti kuhusu
malaria ya shirika la afya duniani (WHO) mwaka 2015, visa vya maambukizi
ya malaria na vifo kutokana na ugonjwa huo vilipungua tangu mwaka 2000.
Ufanisi huenda ulipatikana kupitia utanuzi wa vifaa na nyenzo za kuzuia
na kutibu malaria, kama vile neti za mbu zilizonyunyiziwa dawa, kupima
malaria na utoaji wa dawa ya kuzuia ugonjwa huo.
Takwimu kutoka wizara ya afya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na wastoto zinaonesha kuwa kila mwaka
watanzania wapatao milioni 18 wanaugua ugonjwa wa malaria hali ambayo
inalifanya taifa kupoteza mapato mengi ambapo inakadiriwa kila mwaka
zaidi ya sh. milioni 350 zinapotea kwa ajili ya malaria.
Malaria ni ugonjwa wa
kuambukizana unaoletwa na chembe chembe zinazoitwa plasmodium.Chembe
chembe hizi huingia ndani ya mwili wa binadamu baada ya kuumwa na mbu wa
kike kwa jina Anopheles.
Aidha Mbu mwenye chembe chembe
za plasmodium anapomuuma mtu humuingizia baadhi ya mate yenye viini vya
kuambukizana kwenye kidonda hivyo kusambaza Malaria.
Viini hivyo husafiri hadi
kwenye maini ambapo hukaa hadi vifikie ukomavu na kusababisha homa
inayoandamana na maumivu katika viungo vya mwili, kutokwa na jasho,
kutetemeka, kutapika na kupapatika kama mtu aliye na kifafa.
Katika kuhakikisha kuwa tatizo
hilo linapatiwa ufumbuzi WAZIRI mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anawataka watanzania kuunga
mkono juhudi za Serikali kuutokomeza ugonjwa huo ambao umekuwa chanzo
cha vifo vya watu wengi nchini.
Waziri Ummy anasema Serikali
imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kudhibiti Malaria 2014 –2020 kwa
kushirikiana na afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa
malaria nchini hivyo kupitia afua hizo kiwango cha maambukizi ya malaria
kimeshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2008 hadi 9.2 mwaka 2011/12.
Anasema kuwa mwaka 2014/15
Serikali ilisambaza dozi 12,911,100 za dawa mseto ya kutibu malaria na
vitendanishi vyenye jumla ya vipimo 28,130,736 vya kupima malaria
(mRDT), katika vituo ili kuthibitisha uwepo wa vimelea kabla ya
matibabu.
Anaongeza kuwa vyandarua
vipatavyo 500,000 viligawiwa katika shule za msingi na Sekondari za
Mikoa ya Lindi, Mtwara na shule 24 za mkoa wa Ruvuma kupitia Programu ya
Wanafunzi Shuleni pamoja na kunyunyizia dawa za ukoko ndani ya nyumba
katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na katika nyumba 400,000 za wananchi.
Anaeleza kuwa kuanzia mwaka
2015/16, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya
mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia katika kata za Jiji la Dar es
Salaam pamoja na miji sita iliyofanyiwa maandalizi ya Mpango huo ikiwemo
Miji ya Kibaha, Mwanza, Musoma, Bukoba, Shinyanga na Geita.
“Msisitizo mkubwa wa Wizara
yangu ni kwamba wananchi na wadau wote waone umuhimu na kutoa kipaumbele
katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa kuhakikisha matumizi
sahihi ya mikakati iliyopo katika kuuthibiti ugonjwa huu”anasitiza
Waziri Ummy.
Anasema iwapo mikakati hiyo
itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua
kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa.
Kwa upande wa Tanzania Visiwani
Waziri wa Afya wa Zanzibari Mahmoud Thabit Kombo alisema kuwa Zanzibar
inaadhimisha siku hii kwa kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika kupambana na ugonjwa wa malaria.
Mhe. Kombo anasema kuwa Katika
maadhimisho ya mwaka huu wa 2016, Wizara yake imepanga kutoa elimu kwa
jamii juu ya njia mbali mbali za kijikinga na malaria pamoja na maradhi
mengine ya kuambukiza. Anasema malaria bado ni tatizo kwa upande wa
Zanzibar na katika mikoa yote ikiwemo Wilaya ya Magharibi A na B, Wilaya
ya Kati na Micheweni Pemba.
Anatoa wito kwa wananchi
kuendelea kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kusafisha mazingira
tunayoishi ili kuondosha mazalio, kufunika maji ndani ya mahodhi, mapipa
na sehemu nyengine ili kujikinga na ugonjwa huo na kuzuia fursa ya mbu
kuzaliana.
“Ninatoa wito kwamba mtu yeyote
ndani ya familia anapojihisi kuwa ana homa ni vema akaenda kituo cha
afya kilichoko karibu nae ili kuchunguzwa kama ana homa ya malaria, mtu
asitumie dawa kwa kuhisi dalili za malaria bila kufanyiwa uchunguzi”,
anasisitiza Mhe.Kombo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili
wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho Siku ya Malaria anasema kuwa
Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha
kinga dhidi ya ugonjwa huo na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali
itaendelea kuhakikisha tiba sahihi inapatikana kwa watu wote.
Bw. Juma Hassan mkazi wa
Buguruni mmoja wa waathirika wa Malaria nchini anasema kuwa mazingira ya
Tanzania yamekuwa ni mazalio ya mbu hali inayochangia kueneza ugonjwa
wa malaria ambao unamaliza maelfu ya watu kila mwaka.
Anasema ugonjwa wa malaria
hauwezi kumalizika katika mazingira rafiki kwa mazalio ya mbu, ametolea
mfano baadhi ya maeneo nchini watu wamechimba mabwawa ya kufugia samaki
ambayo hayana samaki badala yale yamekuwa mazalia ya mbu.
“Iwapo katika mabwawa hayo
kungekuwa na samaki, wangekula vimelea vya mbu na kuzuia mbu kuzaliana
pia usafi wa mazingira ungefanyika kikamilifu mazalio ya mbu yangepungua
na hatimaye malaria ingebakia historia’’, alisisitiza.
Siku ya malaria huazimishwa
kila mwaka tarehe 25 Aprili, na kauli mbilu ya mwaka huu ni “Maliza
Malaria Kabisa’ yenye Lengo la kuwakumbusha wananchi katika ngazi zote
kuendelea kupambana na malaria.
No comments:
Post a Comment