Saturday, 16 April 2016

DART YAHIMIZWA KUELIMISHA WAKAZI WA DAR.


Dart4_zps86ebdba6
ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kuanza, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

“Katika kipindi hiki cha majaribio, ambacho madereva wameanza kutumia barabara za BRT, hakikisheni mnatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu namna ya kuvuka barabara, kuzuia wenye bodaboda kutumia barabara hizo kuelezea na matumizi ya taa za barabarani kwa madereva wote,” amesema.
Ametoa agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu aliwataka watendaji wa wakuu wa taasisi wahakikishe wanapanua wigo na kutumia vyombo vya habari vingi kadri iwezekanavyo pamoja na mitandao ya kijamii katika kuelimisha raia juu ya zoezi hilo.
Akifafanua kuhusu hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema miundombinu kwa ajili ya mradi huo imekamilika na usafiri huo utaanza hivi karibuni.
Mhandisi huyo ametumia fursa huyo kutoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu ya barabara hizo kwa sababu imeigharimu Serikali fedha nyingi.
Naye Mrakibu wa Polisi (SP), John Shawa kutoka Makao Mkuu ya Trafiki alisema kuanzia kesho zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka litaanza hivyo amewaomba wananchi kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“Kuanzia kesho linapoanza zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka ni vema watu wakatumia vizuri barabara hasa madereva wa bodaboda na madereva wengine watambue kuwa hawaruhusiwi kupita katika barabara hizo,” alisema

No comments: