Saturday, 16 April 2016

Wafanyakazi ‘waufagilia’ ujenzi Daraja la Kigamboni.

da
Mmoja wa wataalamu wa kizalendo walioshiriki kwenye ujenzi wa Daraja la Kigamboni Muhandisi Jamal Mruma (kushoto) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) namna mradi huo ulivyowajengea uwezo kiutendaji wafanyakazi wazalendo. Kulia ni Meneja wa Mradi huo huo Bw. Zhang Bang Xu.


SIKU chache kabla ya uzinduzi wa daraja la kisasa la Kigamboni, wafanyakazi na wataalamu wazawa walioshiriki kwenye ujenzi wa daraja hilo wamesema kupitia mradi huo wamepata fursa ya kuongeza ujuzi unaowapa mwongozo katika kutekeleza kwa ufanisi miradi mikubwa inayofanana na huo.
Mradi huo uliogharimu Dola za Kimarekani milioni 135 umetekelezwa na  kampuni ya China Railway Construction Engineering Group kwa ushirikiano na kampuni ya China Railway Major Bridge Group ya nchini China.
Wakizungumza kwenye eneo la ujenzi wa daraja hilo jijini Dar es Salaam jana baadhi wa wataalamu na wafanyakazi hao walisema kupitia mradi huo wameweza kujifunza mbinu na teknolojia za kisasa zaidi hatua inayowapa mwanga kuhusiana na utekelezaji wa miradi mikubwa na inayohusisha teknolojia ya kisasa kama huo.
“Mafunzo ambayo tungeweza kwenda kusomea nje ya nchi kwa gharama kubwa tumeweza kuyapata kupitia mradi huu tena kwa vitendo zaidi kwa kuwa tulikuwa tukishirikiana na wenzetu kutoka China bega kwa bega,’’ alibainisha mmoja wa wataalamu hao, Muhandisi Jamal Mruma.
Alitoa wito kwa Serikali na taasisi za elimu ya mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kutumia miradi mikubwa kama hiyo kuwajengea uwezo wanafunzi na wataalamu kutoka vyuo hivyo kupata  mafunzo kwa vitendo.
“Tulipokea baadhi ya wanafunzi kutoka baadhi ya vyuo hapa nchini ikwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  na vyuo vingine waliotembelea kuona mradi na mafunzo mafupi… nahisi tulitakiwa tungechamkia zaidi hii fursa ili waje wengi zaidi,’’ aliongezea
Nae Francis Mambo ambaye ni mkadiliaji ardhi kwenye mradi huo pamoja na kushukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka kwa wenzao kutoka China, alitoa wito kwa serikali na watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanawekeza nguvu nyingi kwenye kujifunza lugha ya kichina kutokana muingiliano wa kijamii na  kiuchumi unaozidi kukua kila siku.
Kwa upande wake Meneja mradi kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group ambao wametekeleza mradi huo kwa ushirikiano na kampuni ya China Railway Major Bridge Group Bw. Zhang Bang Xu alisema mradi huo umehusisha ajira zaidi ya  5000 wakiwemo wataalamu na wafanyakazi huku akionyesha kuridhishwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji ulioonyeshwa na wafanyakazi hao.
“Mbali na daraja hili la kisasa walipatata pia fursa ya kujifunza kutengeneza daraja la awali ambalo lilihusisha teknolojia ya kati ambalo ndio lilitumika katika ujenzi wa daraja hili kubwa,’’ alisema.
Alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kwa kiasi kikubwa kulisababishwa na changamoto zisizotarajiwa ambazo ziliukumba mradi ikiwemo kugundulika uwepo wa pango- hewa chini ya bahari na hivyo kusababisha wao kutumia zaidi miezi sita kujaza pango-hewa hilo.
“Pamoja na changamoto kadhaa tunashukuru tumekamilisha salama mradi huku kwa kiasi kikubwa tukiwa tumefanikiwa kutunza mazingira ikiwemo bahari yenyewe, uoto jirani na bahari pamoja na kubadili hali ya kiuchumi ya wafanyakazi na majirani wanaoishi jirani na mradi,’’ alishukuru.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake leo (JUMAMOSI)  wanatapa fursa ya kulitumia kwa mara ya kwanza Daraja hilo ili kutoa fursa kwa mkandarasi kuhakiki uwezo na ubora wa daraja hilo kabla halijazinduliwa na Rais Magufuli siku Jumanne

No comments: