Mwenyekiti
wa Wabunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, (EALA), Makongoro
Nyerere akifafanua jambo wakati wabunge kutoka EALA walipokutana
na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ulinzi na Usalama
pamoja na Kamati ya Viwanda Biashara na Mazingira jijini Dar es Salaam
leo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kadumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalali Kafumu.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Twaha Taslima
akifafanua jambo mbele ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo
ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara
na Mazingira jijini Dar es Salaam leo.
Wabunge
wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala) wameomba
ushirikiano kutoka kwa wabunge wenzao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika kusaidia kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu
fursa za mtangamano (integration) wa Jumuiya.
Mwenyekiti
wa wabunge wa Tanzania katika EALA, Makongoro Nyerere, aliwaambia
wabunge wa kamati za Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na ile ya Viwanda,
Biashara na Mazingira katika kikao cha pamoja jana jijini Dar es Salaam
kuwa miongoni mwa fursa zitokanazo na mtengamano wa Afrika Mashariki ni
pamoja na zile za biashara na masoko.
Akizungumza
kwa niaba ya wabunge wenzake tisa wa EAlA, Makongoro alizitaja fursa
nyingine kuwa ni za elimu, uwekezaji, ajira na kujiajiri, kwenda popote
katika Jumuiya, uhuru wa kuishi popote katika nchi wanachama kwa wale
wenye shughuli maalum, kuboreshwa kwa miundombinu, maonesho ya
wajasiriamali na maonesho ya utamaduni na fursa zinazotolewa kwa familia
(Dependants).
Alisema
Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inajengwa
katika mfumo wa ushindani wa soko na kwamba kila fursa iliyopo katika
Jumuiya inapatikana kwa ushindani miongoni miongoni mwa wananchi wa nchi
wanachama.
“Hivyo,
Watanzania kama raia wa nchi zingine wanachama ni lazima wachangamkie
fursa na kuzitumia. Ili kushindana, Watanzania wanatakiwa kujiamini na
kuacha kujiona wanyonge ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani akili
tunazi, uwezo tunao na nguvu tunazo,” alifafanua.
Akichangia
katika mkutano huo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula,
alisema ni vema elimu kuhusu mtangamano wa Afrika Mashariki, hususan
kuhusiana na fursa za kibiashara, ikatolewa pia kwa wafanyakazi wa
taasisi zinazofanya kazi kwenye maeneo ya mipakani, kama vile Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa kikwazo kwa
wafanyabiashara kutokana na utendaji wao usioridhisha.
Alisema
watumishi katika vituo vya mipakani wamekuwa wakiwakatisha tamaa
wananchi wanaofanya biashara kiasi cha kuwafanya waendelee kutumia njia
za panya.
Naye
mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema) alisema Tanzania bado
ina kazi kubwa katika ushindani ndani ya Jumuiya akitolea mfano wa Kenya
ambayo imefikia uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda vya kutosha wakati
nchi yetu ndio inafikiria kufufua na kuanzisha viwanda.
Alisema
kuna hatari ya Tanzania kubakia kuwa soko wakati nchi kama Kenya
zinapambana kufanya uzalishaji mkubwa wa viwandani na kuimarisha ubora
wa bidhaa zake.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu
aliwataka Watanzania kutafuta mbinu za kuwa wabunifu zaidi katika
ushindani ndani ya Jumuiya ili kuweza kufanikiwa kukamata fursa za
mtangamano.
Wabunge
wa Afrika Mashariki ambao wapo katika shughuli za kuhamasisha na
kuelimisha umma kuhusu fursa za mtangamano wa Afrika Mashariki wamesema
siku za usoni wanatarajia kufanya mkutano na wabunge wote ili
kubadilishana nao uzoefu kuhusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki
No comments:
Post a Comment