Kuna tiba nyingi za kitabibu, zilizogawanyikaa katika makundi
mbalimbali. Kuna zile za hospitali ambazo ni lazima zinunuliwe, lakini
kuna tiba ambazo kwa ushauri wa daktari hata wewe unaweza kuziandaa bila
kutumia gharama kubwa.
Moja ya tiba hizo ni kunywa maji ya moto. Kwa mujibu wa wataalamu wa
afya maji moto yanatibu magonjwa mengi ikiwemo: Figo, kutoa sumu
mwilini, kuyeyusha mafuta tumboni, kurahisisha mzunguko wa damu, kuondoa
sumu kwenye ubongo na kusafisha haja ndogo.
Kunywa maji ya moto kila unapotaka kwenda kufanya kazi ya nguvu au
mazoezi iwe kama kinga na inashauriwa kila siku anywe glasi nane ili
kutoa taka na kila kisichotakiwa kubaki mwilini, kupitia jasho.
Wadau wa afya wanasema kuwa ni vyema pia kunywa maji ya moto yenye
ndimu au limao kabla ya kifungua kinywa ili kurahisisha mfumo wa mwili
kwa siku nzima.
Pazi Mwinyimvua, Mtaalamu wa Chakula na Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, anasema kuwa maji yanarahisisha uyeyushaji wa chakula na
mafuta mwilini, hivyo kutokana na umuhimu huo ni vyema kunywa maji ya
moto yatakayofanya kazi haraka na kwa ufanisi mkubwa bila kuchosha figo.
Anaitaja faida nyingine ya kunywa maji ya moto kuwa ni kutoa sumu
zilizopo kwenye mishipa ya fahamu na kuisaidia figo kufanya kazi
kikamilifu, tofauti na maji baridi ambayo yanagandisha na kuilazimisha
figo kuyeyusha kwanza na kisha kuchuja
Anashauri umuhimu wa kunywa maji moto kabla ya kufanya mazoezi kuwa ni
kujiandaa kwa ajili ya kuchuja jasho ambalo litatoa sumu, hivyo yakiwa
ya moto yakifika yanaanza kufanya kazi moja kwa moja, kuliko yakiwa ya
baridi yanaweza kusumbua kwa kuwa ni lazima yapate joto la mwili kwanza
kabla ya kuanza kufanya kazi.
“Ukiachilia kusubiri yachemke pia ni kumuepusha mtumiaji na hatari ya
kuumwa tumbo kutokana na kunywa maji ya baridi bila kuweka kitu tumboni
na kwenda kufanya mazoezi kitu kinachoweza kuzidisha maumivu au maji
kucheza wakati wa kukimbia kama mazoezi ya kukimbia. Lakini yakiwa ya
moto ni kama umekunywa chai au kula chakula cha kawaida” anasema
Mwinyimvua.
Mwinyimvua anaongeza kuwa maji ya moto ni mazuri hata kwa kupata choo,
kwa vile kinarahisisha uyeyushaji na uchambuaji wa kinachotakiwa na
kisichotakiwa, wanaokunywa ya baridi wana uwezekanao mkubwa wa kupata
haja kubwa kwa shida.
Vilevile Mwinyimvua anashauri kuwa ni vyema kunywa maji moto
yaliyochemshwa na kuyaacha yapoe na kuwa vuguvugu na kuongeza limao na
asali mbali na kuongeza ladha, asali na limao vina faida kiafya.
Gayl Canfield , RD, Mkurugenzi wa Lishe kutoka katika Kituo cha Biashara
cha Pritikin Longevity kwenye Mji wa Miami , Florida nchini Marekani,
anasema kuwa kunywa maji ya uvuguvugu au ya moto ni vyema kwa kuwa
hufanya kazi moja kwa moja kutokana na hali ya tumbo kuwa na joto muda
wote.
Canfield anasisitiza, “Maji ni muhimu kwa mwili wako, yakiwa ya moto
ni bora zaidi, kwa kuwa yanatoa rangi ya njano ya mkojo na kuufanya uwe
msafi na wenye rangi angavu”.
Anasema maji ya moto yanaweza kukusaidia kupoteza uzito au kudumisha uzito ulionao sasa.
“Maji ya moto yanaweza kuongeza joto la mwili na hivyo kuongeza
kiwango ufanyaji kazi wa mwili kidogo, “ anasema Dk Michael Wald ,
Mkurugenzi wa Huduma za lishe katika kituo cha Integrated kilichopo New
York, Marekani.
Anasema ili mwili ufanye kazi ipasavyo husaidia utumbo na figo kufanya
kazi kwa ufanisi zaidi. Kunywa maji ya moto pia husaidia kupunguza uzito
wa mwili na kuwa na nuru na siyo kusinyaa. Vilevile huchangamsha
utendaji kazi wa ubongo.
Dk Michael Wald anaitaja faida nyingine ya kunywa maji ya moto kuwa ni
kujenga mazoea ya kuchemsha maji hivyo kupunguza idadi ya maambukizi
yanayotokana na kunywa maji bila kuchemsha.
“Maji baridi hugandisha mafuta ndani ya miili yetu, ikiwa ni pamoja na
mishipa ya damu,hali hii ikiendelea inaweza kusababisha shinikizo la
damu kutokana na ukosefu wa mzunguko wa damu pamoja na magonjwa mengine
mengi. Kama haikufanyiwa kazi inaweza hata kusababisha saratani ”
anasema Dr Michael Wald .
Mganga Mkuu Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela, anasema kuwa
kunywa maji ni muhimu yawe baridi au ya moto na hakuna sababu za
kitaalamu zinazohusisha na dawa au kutibu kitu chochote.
Anasema, watu wa tiba mbadala ndiyo wamelikuza hilo lakini kitaalamu
halipo na kunywa maji ni muhimu kwa kila mtu bila kujali ni ya moto au
baridi, hayo mengine ni maneno tu.
“Watu wanashauriwa kunywa maji ya moto kwa wale wasiopenda kunywa maji,
kwa kuwa yakiwa ya uvuguvugu inakuwa nafuu kwao kunywa na wengine
huambiwa waweke ndimu au limao siyo kama dawa bali kuyapa ladha ili
waweze kunywa” anasema Shimwela.
Anaendelea kufafanua kuwa kama kuna wanaodharau kunywa maji wakiona ni
kitu kidogo wanakosea sana kwa kuwa maji ni msaada hata unapopata tatizo
la kiafya.
Anasema kuwa hata katika usagaji wa chakula maji husaidia, hivyo kama mhusika amekunywa maji atarahisisha kitendo hicho.
Dk Raymond Mwenesano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kuwa
kunywa maji ni muhimu kwa kila mwanadamu ili kurahisisha utendaji wa
mwili ikiwamo mzunguko wa damu bila kujali ni moto au baridi.
Dk Mwenesano anazitaja faida za kunywa maji moto kuwa ni : Kuboresha
uyeyushwaji wa chakula. Maji ya vuguvugu yakiwekwa limao, yanasaidia
usafishaji wa tumbo, kuondoa sumu mwilini kupitia jasho, kusafisha pua
na koo, kuboresha mzunguko wa damu , husaidia upatikanaji wa haja kubwa,
kuongeza kinga mwilini endapo asali na limao vitaongezwa.
No comments:
Post a Comment